KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, October 28, 2010

Kanisa halimpigii debe mgombea yeyote-PCT



Exuper Kachenje
BARAZA la Makanisa ya Pentekoste (PCT) limeeleza kuwa hakuna mgombea ambaye anapewa kipaumbele na baraza hilo kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili.

Lakini katika tamko lake, PCT imeitaka Tume ya Uchaguzi (Nec) kusimamia kwa haki uchaguzi mkuu na kutoa haki bila kupindisha, likisema kuwa jaribio lolote la kuupindisha ukweli ni hatari kwa amani ya Taifa.

Akizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari jana, mwenyekiti PCT, Askofu David Batenzi alisema pia kuwa baraza hilo linapinga msimamo wa udini na ukabilia katika kupata kiongozi wa ngazi yoyote.
“PCT inatoa tamko kwa umma wa Watanzania kwamba haina chama au mgombea anayepewa kipaumbele au kupigiwa kampeni ndani ya umoja wake katika uchaguzi mkuu wa 2010,” alisema Batenzi.

Askofu huyo mkuu alifafanua kuwa “PCT inasisitiza Wakristo na Watanzania wote kuchagua kiongozi yoyote mwenye uwezo, mwadilifu na mwenye nia ya kujenga umoja, amani na utulivu wa Watanzania bila kujali itikadi, rangi au imani ya mgombea”.
Katika mkutano huo ambao ulijumuisha viongozi wengine wa kanisa hilo, Askofu Batenzi alisema tamko hilo limetolewa kwa niaba ya makanisa wanachama wote wa PCT na kwamba PCT inaheshimu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanazania.
Alisema: “PCT inaheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kwamba ni haki ya kila mwananchi kuchagua au kuchaguliwa kwa nafasi yoyote ya uongozi bila kuangalia dini, kabila au rangi yake.”

Kwa mujibu wa askofu huyo, misingi ya uadilifu, ukweli, uzalendo, umoja, amani na utulivu ndiyo kipimo pekee cha kutumiwa na mwananchi katika kujichagulia kiongozi wanayempenda bila kushurutishwa na mtu au kikundi fulani.
Akieleza sababu za tamko hilo, Askofu Batenzi aliwaambia waandishi kuwa PCT inataka kuweka bayana msimamo wake dhidi ya wananchi kuchagua vionghozi kwa misingi ya kidini na kikabila.

Kuhusu Nec, askofu Batenzi alionya kuwa “ni vizuri Tume ya Uchaguzi isimamie kwa haki uchaguzi huo na itoe matokeo kwa haki kwa kadiri yatakavyokuwa kwa kuwa kupindisha matokeo ni hatari kwa amani ya taifa”.
Aliwataka wagombea kuwa tayari kukubali matokeo na kutokuwa chanzo cha uchochezi na vurugu huku akiwataka Watanzania pia kuwa watulivu baada ya upigaji kura na kukubali matokeo kwa faida ya amani iliyopo nchini

No comments:

Post a Comment