KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, October 28, 2010
Kikwete aahidi neema Mwanza
Frederick Katulanda, Mwanza na Kizitto Noya, Nyang’hwale
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amesema ataipandisha hadhi Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure kuwa ya rufaa na kuongeza fedha kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando, huku akiahidi kujenga jengo kubwa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Alisema tayari hospitali hiyo imeshafanyiwa marekebisho ikiwa ni pamoja na kujengewa wodi maalum ya magonjwa ya akili, kuongezwa wodi ya akinamama na maabara kama sehemu ya mkakati huo wa kuboresha huduma ya afya.
Akizungumza jijini Mwanza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Sahara Jimbo la Nyamagana jijini Mwanza, Kikwete alisema hospitali hiyo imeboreshwa kwa lengo la kutoa huduma bora na kuifanya ifikie ngazi ya rufaa.
“Tayari tumeshaweka vifaa vya kisasa na maabara; tunataka ndiyo iwe ya rufaa na ile ya rufaa ya Bugando tutaifanya kuwa ya rufaa maalum,” alisema Kikwete na kubainisha kuwa katika mpango huo tayari serikali imepanga kutoa Sh8 bilioni kwa ajili ya kuiwezesha Bugando kununulia vifaa maalum vya upimaji.
Kikwete alisema iwapo CCM itachaguliwa tena, mpango wao ni kujenga kituo cha Machinga Complex pamoja na soko kubwa la kisasa jijini Mwanza na soko la zamani libaki kama historia na kubeza ahadi za upinzani akidai kuwa zinatolewa na watu ambao hawana hata viwanda.
“Tumefanya mengi... nawaomba msibabaike na ahadi hewa za wapinzani ambazo wanazitoa kuwa watashusha bei ya vitu wakati hata viwanda hawana,” alieleza Kikwete.
Akizungumzia fujo katika kampeni, Kikwete alisema CCM ni waaminifu kwa kuwa waliahidi amani na amani ipo na kusema kuwa ni CCM pekee inayohubiri amani huku akisema wapinzani wamekuwa wakiahidi fujo.
“Wanafanya fujo; wanapiga watu; wanajeruhi watu na sasa wameua... achaneni nao hao kwa kuwa ukiona mtu anafanya fujo, ujue kuwa amekata tamaa. Kama CCM tungekuwa wabaya, tusingeruhusu vyama vingi; tungevinyongea mbali, lakini tumewaruhusu sasa wanafanya fujo. Siasa siyo kupigana mawe ni sera; waje na sera,” alieleza Kikwete.
Kikwete amekuwa akidaiwa kufuja fedha kwa kusafiri nje kila mara, lakini jana alijitetea kuwa safari hizo ndizo ambazo zimeleta mafanikio, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa serikali ya Marekani kusaidia vyandarua.
“Wapo watu wanasema natembea sana; hivi nisingetembea ningempata wapi (rais wa zamani wa Marekani, George) Bush atuletee vyandarua na vitabu kwa ajili ya shule zetu. Tumegawa vyandarua kupitia hati punguzo na sasa tutagawa zaidi kwa lengo la kuhakikisha kila kitanda kinakuwa na chandarua kwa nchi nzima,” alisisitiza Kikwete.
Alisema tatizo la walimu katika sekondari za kata litamalizika kwa kuwa serikali yake imefundisha vijana 14,000 ambao watahitimu mwaka huu na kusambazwa katika shule hizo, akiahidi kuipa kila shule walimu watano.
Alieleza kuwa serikali yake imekuwa tulivu na sikivu na kila inapoahidi imekuwa ikitimiza na akawaomba wananchi kumchagua tena ili aweze kukamilisha aliyoahidi kwao.
Akihutubia mkutano Nyanghwale, Kikwete alieleza kuwa serikali yake inatambua tatizo la umeme katika jimbo hilo na imejipanga kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema CCM inaomba kura ili ichaguliwe tena kurudi madarakani kwa sababu kadhaa "kubwa ni kwamba CCM ni chama makini, chenye sera nzuri na kinachojali mahitaji ya wananchi wake”.
Pia alisema serikali itajenga barabara ya lami kutoka Geita, Kahama, Nyang’hwale ili kumaliza tatizo la miundombinu ya usafiri katika eneo hilo.
Aliahidi kumaliza tatizo la benki akisema kuwa “tutazungumza na watu wa mabenki kuwaomba waanze kufungua matawi katika jimbo hili”.
“Ninaposema mtuchague, nina maana kuwa mimi kwa nafasi ya urais, Amar kwa nafasi ya ubunge na wagombea wetu wa udiwani,” alisema na kueleza kuwa anaamini Amar ana uwezo mkubwa wa kuliongoza jimbo hilo kwa mafanikio ya kweli.
Awali kabla hajaingia uwanjani, pikipiki takribani 65 zilizopambwa bendera za CCM na baiskeli kadhaa zilikuwa moja ya vivutio katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyang’hwale lililoko Kata ya Karumwa wilayani Geita, Mwanza.
Kikwete aliyefika kwenye uwanja huo majira ya saa 10:30 jioni, alianza kuhutubia baada ya mgombea ubunge, Hussein Nassor Amar kueleza matatizo kadhaa yanayolikabili jimbo hilo.
“Mheshimiwa mwenyekiti wa CCM na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ujio wako leo ni faraja kubwa kwa wakazi wa jimbo hili ambalo kwa mara ya mwisho rais alifika mwaka 1972,” alisema Amar.
“Jimbo hili lina matatizo mengi, lakini kubwa ni ukosefu wa umeme, maji na miundombinu ya mawasiliano. Pia katika jimbo hili kuna mzunguko mkubwa wa fedha, lakini hakuna benki. Tunaomba utusaidie kupata benki ili kuwapunguzia muda wa kwenda wilayani watumishi wa umma.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment