KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, October 28, 2010
JK atangaza kumaliza tatizo la maji umasaini
digg
Kizitto Noya, Simanjiro
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete jana aliendelea na kampeni katika Jimbo la Simanjaro ambako pamoja na mambo mengine, aliahidi kutafuta Sh30 bilioni kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji kwenye jamii hiyo ya wafugaji.
Akizungumza kwenye viwanja vya Orkesumet, makao makuu ya Wilaya ya Simanjiro, Kikwete alisema mbali na kumaliza tatizo hilo, serikali yake ijayo pia itatoa ruzuku ya dawa ya josho za ng’ombe kwa wafugaji.
“Jitihada za awali za tatizo la maji tayari zimeelezwa na mbunge wenu (Ole Sendeka) lakini serikali inajipanga kumaliza kabisa tatizo hilo," alisema Kikwete.
“Tunahitaji kuwa na Sh30 bilioni kwa ajili ya kuvuta maji kutoka Mto Ruvu na huu ni mradi mkubwa ambao mipango ya awali ya kuomba fedha imeshaanza.”
Kwa mujibu wa Kikwete, wakati serikali inaendelea kusubiri Sh30 bilioni, jitihada za awali zimeanza kwa kutenga Sh1.8 bilioni kwa ajili ya kuchimba visima virefu vya maji.
“Tutachimba visima hivyo kwa awamu. Tutaanza na vijiji 12 na baadaye vijiji vingine vilivyobaki,” alisema Kikwete ambaye pia alieleza kuwa lengo la serikali yake ijao ni kumaliza kabisa tatizo la maji nchini.
Kikwete alisema maelekezo ya CCM kwa serikali ijayo, ni kuhakikisha inatengeneza mipango ya kuendeleza sekta za maji, mifugo na kilimo na yeye kama msimamizi mkuu wa maelekezo hayo, amejipanga ipasavyo kuhakikisha hilo linafanikiwa.
“Tuchagueni tuendelee kustawisha nchi yetu. Tutahakikisha kila mfugaji anakuwa na maji yake katika kipindi chote cha mwaka ili kuondokana na tatizo la kuhamahama,” alisema
Awali kabla ya Kikwete kuanza kuhutubia, mbunge anayetetea nafasi yake kwa tiketi ya CCM jimboni humo, Christopher Ole Sendeka alimkabidhi rungu na mgolole kama ishara ya ushindi na uongozi.
Baadaye mbunge huyo mteule alisema CCM ni chama kinachostahili kuendelea kuongoza nchi kwani kimefanya mengi katika kipindi kifupi cha miaka mitano iliyopita chini ya uongozi wa Kikwete.
“Katika kipindi hicho cha miaka mitano, makao makuu ya Simanjiro ya Orkesumet hayakuwa na umeme, lakini sasa tumefanikiwa kusambaza umeme,” alisema Ole Sendeka.
“Katika kipindi hicho pia tumechimba visima 55 virefu vya maji na kuongeza idadi ya wanafunzi wa sekondari kutoka 180 hadi 2,300. Tumeongeza pia shule kutoka tatu hadi 16 na kufanikiwa kutengeneza barabara ya Simanjiro hadi Arusha,” alisema
Rais Kikwete jana alifanya kampeni katika majimbo ya Kiteto, Simanjiro na Karatu kwa mpinzani wake wa urais, Dk Willibrod Slaa.
Tathimini inaonyesha kuwa Kikwete atapata kura nyingi zaidi kuliko wagombea wengine wa vyama vya upinzani katika jimbo la Simanjiro hasa baada ya ole Sendeka kupita bila kupingwa huku CCM ikipita pia bila kupingwa katika kata 16 kati ya kata 18 za jimbo hilo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment