KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, October 28, 2010

CCM yataka wanachama wasitembee na visu Jumapili




digg
Ally Mkoreha na Sadick Mtulya, Zanzibar
CCM visiwani Zanzibar ,imewataka wanachama wake kutotembea na silaha ya aina yoyote katika siku ya kupiga kura. Pia kimewataka wasichokoze wala kuchokozeka na watu watakaojaribu kuwachokoza.

Kimesema kufanya hivyo, kutasaidia kuufanya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kote nchini Jumapili ijayo, kuwa wa amani.

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM visiwani Zanzibar , Salehe Ramadhan Feruzi, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama hicho, uliofanyika katika Jimbo la Dole, Mjini Magharibi.

Mkutano huo ulihutubiwa na mgombea mwenza wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk Mohamed Gharib Bilal.

“Ndugu zangu nachukua nafasi hii tuwekane sawa kuhusu siku ya kupiga kura. Tunaomba wanachama na wafuasi wa CCM siku hiyo wasitembee na okapi (visu) na wala tusivae sare au kutembea na kitu chochote chenye nembo ya chama chetu,” alisema Feruzi kabla ya kumkaribisha Dk Bilal kuhutubia.

Pia aliwataka wahimizane na kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura, ili kukiwezesha chama chao kuibuka na ushindi.

Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM, Shamsi Vuai Nahodha, alisema ushindi wa CCM ni wa lazima na kwamba hiyo inatokana na ukweli kwamba chama hicho kina sera zinazokubaliwa hata na wapinzani.

“Lakini pia matukio mawili ya hivi karibuni, pia yanaashiria ushindi mkubwa wa CCM. Viongozi wakubwa wawili wa CUF walikiagaa chama chao na kujiunga na CCM. Lakini pia kule Mwanakwerekwe watu wazima walilishana chakula hadharani. Hii ni ishara kubwa ya ushindi wa CCM,” alisema Nahodha ambaye pia ni Waziri Kiongozi anayemaliza muda wake katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea (Bilal), aliwataka wanachama wa CCM wajipange na kuhakikisha kuwa siku ya kupiga kura, wanawachagua Jakaya Kikwete kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk Ali Mohamed Shein, kuwa Rais wa Zanzibar .

“Mimi nimeshalala kwenye zaidi ya vitanda 63 nikiomba kura nchi nzima. Nanyi nakuombeni mtumie lugha laini hata kwa wapinzani wetu, kuomba kura, msiwaogope,” alisema Dk Bilal.

Alisema Kikwete na Shein, wamejipanga kuiletea Tanzania maendeleo na kuhakikisha kuwa amani ya nchi inaendelea kudumu.

“CCM tayari imeshajipanga kuwarithisha vijana amani kama ilivyowarithisha viongozi walioko madarakani ambao hawana hasira, chuki na ni watulivu,” alisisitiza Dk Bilal ambaye hata hivyo hakutumia muda mrefu kuhutubia.

No comments:

Post a Comment