KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, September 20, 2010

Papa akutana na waliodhalilishwa na mapadre

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Benedict, akiwa ziarani nchini Uingereza amekutana na kundi la watu waliodhalilishwa na makasisi wa kanisa hilo katika miaka ya nyuma, na kuelezea huzuni kubwa na fedheha kuhusiana na waliyoyapitia watu hao pamoja na familia zao.




Papa Benedict akiongoza ibada kwenye bustani ya Hyde Park jijini London.


Alifanya sala na waathirika hao, na kuwahakikishia kwamba kanisa Katoliki linaendelea kutekeleza hatua muafaka zinazokusudiwa kuwalinda watoto.

Alisema kanisa linafanya kila liwezalo kuchunguza madai yote, na kushirikiana na serikali mbali mbali kuona kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya mapadre waliohusishwa na uhalifu huo.

Mapema kwenye misa katika kanisa la Westminster Cathedral kiongozi huyo wa Katoliki aliomba msamaha kwa waathirika wote na familia zao, na kuelezea huzuni kubwa.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Papa Benedict kuomba msamaha hadharani kuhusiana na vitendo hivyo.

Pia alikutana na kundi la watu waliopewa jukumu la kuwalinda watoto kutokana na vitendo kama hivyo vya kudhalilishwa kimapenzi.

Jumamosi jioni zaidi ya watu 80,000 wengi wao waumini wa Katoliki walijumuika katika bustani ya Hyde Park jijini London kwa maombi yaliyoongozwa na Papa Benedict mwenyewe.

Malalamiko

Kulikuwa na maandamano makubwa mjini London ya watu waliopinga ziara ya Papa Benedict huku wakibeba mabango ya kumbeza kiongozi huyo wa Katoliki.

Wengi walielezea ghadhabu kuhusu mapadre kuwadhalilisha watoto kingono, baadhi wakiwa wamevalia fulana zenye maandishi ya kutaka Papa Benedict akamatwe.

Waandamanaji hao pia wamekuwa wakipinga msimamo wa kanisa kukataza ndoa za watu wa jinsia moja, kukataa kutawazwa wanawake kuwa mapadre na kukataza watu kutumia mbinu za uzazi wa mpango.

Kulikuwa pia na watu wasiotaka kujihusisha na dini, ambao waliandamana kupinga ziara hiyo kugharamiwa na serikali kwa fedha za walipa kodi.

Msimamo na mikutano

Kwenye hotuba zote alizotoa katika ziara yake, Papa Benedict alisisitiza haja jamii ya waingereza kukumbuka misingi yao ya kikristo na kukataa wimbi la kampeni za kutaka sherehe za kidini kama vile Krisimasi zipigwe marufuku.

Alitaka imani ya Kikristo ipewe nafasi yake katika shughuli za kila siku nchini Uingereza, na akataka kanisa liendeleze mafundisho yake bila kukabiliwa na hatari ya kutengwa.

Alikutana na Waziri mkuu David Cameron na naibu wake Nick Clegg, pamoja na kaimu kiongozi wa upinzani Bi Harriet Herman.

Papa Benedict pia alikutana na kiongozi wa kanisa la Anglikana duniani, Askofu mkuu Rowan Williams, kama ishara ya maridhiano kati ya makanisa hayo mawili, miaka 500 tangu Uingereza ilipojitenga na Rome.

Kwenye mazungumzo yao alitoa wito wa kuwepo ushirikiano siyo tu baina ya makanisa, lakini pia baina ya dini zote, ili kulinda imani na kuikabili hali inayojiri ya watu kutotaka kujihusisha na imani katika Mwenyezi Mungu.

Kwenye bustani ya Hyde Park Papa Benect aliwaasa waumini wa Katoliki wawe tayari kudhihakiwa kwa ajili ya injili ya Kristo



Papa amekutana na viongozi wa ngazi za juu wa kidini na kiserikali. Hapa yuko na David Cameron, Waziri mkuu wa Uingereza.


Makundi ya waumini wa Katoliki kutoka nchi mbali mbali na parokia nchini Uingereza yalibeba bendera za nchi yao na mabango ya kumkaribisha Papa Benedict.

Kulikuwa na vikundi vya kutumbuiza yakiimba nyimbo kutoka sehemu mbali mbali za dunia mkiwemo zile za Kiswahili za ‘’Moto umewaka’’ na ‘’Twatembea katika mwangaza.’’

Ilikuwa rahisi kuwatambua waumini wa Katoliki kutoka Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuwa walipeperusha bendera za nchi zao na kuvalia mavazi ya Kiafrika.

Papa Benedict anakamilisha ziara yake siku ya Jumapili, ambapo ataongoza misa ya hadhara katika bustani ya Crofton House mjini Birmingham

No comments:

Post a Comment