KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, September 16, 2010

Hatimaye Goodluck Jonathan atangaza nia

Baada ya miezi kadhaa ya tetesi rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametagaza na kuthibitisha kuwa atagombea urais katika uchaguzi wa mwakani.



Goodluck Johnathan atawania urais wa Nigeria


Ametangaza nia yake hiyo kupitia mtandao kwenye ukurasa wake wa Facebook, akisema uamuzi huo umefikiwa "baada ya majadiliano marefu".

Bw. Jonathan, ambaye anatokea eneo la kusini mwa nchi hiyo, aliingia madarakani mwezi Februari kufuatia kifo cha rais Umaru Yar'Adua.

Chama kinachotawala siku za nyuma kiliwahi kusema mgombea lazima atoke eneo la kaskazini mwa nchi.




Ibrahim Babangida

Taarifa ya rais huyo kwenye ukurasa wa Facebook imesema, atatangaza rasmi nia yake ya kuwania urais siku ya Jumamosi.

Wasaidizi wake hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia jambo hilo.

Tangazo hilo limekuja, wakati mmoja wa mahasimu wake wakuu katika chama tawala, PDP, kiongozi wa zamani wa kijeshi Jenerali Ibrahim Babangida akizindua kampeni yake.

Shirika la habari la Reuters limesema maelfu ya watu walikusanyika katika mkutano wa hadhara wa kuzindua kampeni hiyo mjini Abuja.




Vigogo kadhaa wanatarajiwa kujitokea kupitia chama hicho.

Chama cha PDP kina utamaduni wa kupokezana madaraka, kati ya wanaotokea Kusini na Kaskazini, kwa mihula miwili kila upande.

Chini ya kanuni hiyo ambayo si rasmi, mgombea wa mwaka 2011, anatakiwa kutoka upande wa kaskazini wenye Waisilam wengi, na sio upande wa Kusini wenye Wakristo zaidi na watu wenye imani nyingine



Ramani ya Nigeria


Upande wa kaskazini ungependa kumuunga mkono zaidi Jenerali Babangida, au makamu wa rais Atiku Abubakar, kuliko Bw. Johnathan.

Bw. Jonathan ni rais wa kwanza kutoka eneo la kusini la Delta lenye mafuta mengi.

Hata hivyo taarifa yake hiyo imesema, alikutana na kufanya mashauriano na watu nchi nzima, kabla ya kuamua kuwania kiti hicho.

Uchaguzi wa hivi karibuni wa Nigeria umezongwa na ghasia na udanganyifu.

Bw. Jonathan ameahidi kuleta mabadiliko katika tume ya uchaguzi, lakini waandishi wa habari wanasema itakuwa vigumu kutekeleza mabadiliko makubwa kabla ya Januari

No comments:

Post a Comment