KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 16, 2010

Uchunguzi huru wa kifo cha Chebeya washinikizwa

Makundi ya kutetea haki za binadamu barani Afrika yametuma barua kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila, yakimhimiza kuanzisha uchunguzi huru kuhusiana na mauaji ya mwanaharakati mmoja nchini humo.

Floribert Chebeya aliyesifika na kuheshimiwa sana nchini Congo alipatikana ameuawa garini mwake mwezi Juni mwaka huu saa chache bada ya kuwa na kikao na mkuu wa polisi.

Msemaji wa shirika la Open Society Initiative for Southern Africa Hubert Tshiswaka akizungumza kwa niaba ya mashirika hayo amedai kuwa uchunguzi wa awali ulioendeshwa na serikali haukufichua chochote na inaonekana kuwa serikali ilipania kuficha ukweli.

Marehemu Chebeya aliyefariki akiwa na umri wa miaka 47 alikuwa kiongozi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Voice of the Voiceless na wanaharakati wanasema alikuwa akipokea vitisho kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la Amnesty International, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Congo wamekuwa wakiteswa sana huku baadhi wakitishwa na hata kukamatwa kiholela.

No comments:

Post a Comment