KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Monday, August 2, 2010
Sudan yaiwekea masharti askari wa UN
Sudan imesema imewaagiza wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika jimbo la Darfur kuarifu utawala mjini Khartoum kuhusu mipango yao yote ya safari.
Msemaji wa serikali Rabie Abdelati alisema Umoja wa Mataifa ulishindwa kudumisha usalama wa kambi za wakimbizi katika eneo hilo.
Kuanzia sasa mizigo ya walinda amani itakaguliwa kwenye viwanja vyote vya ndege, na wanapaswa kuijulisha serikali ya Sudan kabla ya kusafiri, hata kama ni ndani ya miji.
Siku ya Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwaongezea muda wa mwaka mmoja askari hao wa kulinda amani.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu wanaokisiwa 300,000 wameuwawa Darfur na wengine zaidi ya millioni 2.6 waliachwa bila makao tangu waasi wa kikabila kuanza kupigana mwaka wa 2003.
Serikali ya Sudan inasema idadi ya waathiriwa imetiwa chumvi.
"Kuheshimu uhuru wa Sudan"
Siku ya Jumamosi, watawala katika Darfur Kusini waliwataka wanajeshi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika (UNAMID) kuratibu harakati zao zote na vikosi vya usalama vya Sudan.
Mwandishi wa BBC amesema haijabainika ikiwa hatua hii inamaanisha kuweka masharti kikamilifu kwa jinsi walinda amani hao wanavyotekeleza majukumu yao.
Msemaji wa UNAMID alisema hana habari kuhusu kanuni hizo mpya.
Bw Abdelati, ambaye ni afisa mwandamizi katika wizara ya habari ya Sudan, alisema askari hao wakulinda amani kuanzia sasa hawawezi kuepuka kufuata taratibu za kawaida kwenye uwanja wa ndege wa mjini Nyala katika Darfur Kusini.
Aliongeza kuwa UNAMID ilitakiwa kuwakabidhi katika muda wa saa 48 "wahalifu" watano, ambao alisema walipatiwa hifadhi na jeshi hilo kufuatia mapigano katika kambi kubwa ya wakimbizi ya Kalma, karibu na Nyala.
"UNAMID haikutekeleza majukumu yake ipasavyo - kulikuwa na ufyatulianaji wa risasi, nyumba kuchomwa, na watu kufariki na kile walichokifanya ilikuwa ni kutazama tu" alisema Bw Abdelati, akiongeza kuwa yeye mwenyewe alikuwa Darfur Kusini wakati wa mapigano
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment