KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 31, 2010

Kura ya maoni yafanyika Zanzibar

Kura ya maoni inafanyika Zanzibar hii leo, ambayo inalenga kubadili katiba na kuruhusu uundwaji wa serikali za kuwagawana madaraka.

Zaidi ya wapiga kura laki nne walioandikishwa rasmi wanatarajiwa kupiga kura zao.

Chama tawala CCM na chama kikubwa cha upinzani CUF, vyote vinaunga mkono kura hiyo, ambayo inanuiwa kumaliza ghasia zilizokumba uchaguzi wa siku za nyuma visiwani Zanzibar.
Zanzibar ina utawala wake wa ndani chini ya serikali kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ikiwa kura hiyo ya maoni itapitishwa, Zanzibar kwa mara ya kwanza itashuhudia mfumo mpya wa serikali ambapo kutakuwa na rais na makamu wake wawili.
Makamu wa kwanza wa rais atatoka chama ambacho kitashika nafasi ya pili katika uchaguzi na wa pili atatoka chama kilichoibuka mshindi.

Pia baraza la mawaziri chini ya mfumo huo mpya litakuwa ni la kugawana madaraka.

Mwandishi wa BBC aliyeko Zanzibar anasema matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kutangazwa katika muda wa siku moja.

Baraza la wawakilishi

Baada ya wiki moja, baraza la wawakilishi nalo litakutana ili kufanya marekebisho ya katiba kulingana na matokeo ya kura hiyo ya maoni.

Zanzibar ambayo inaundwa na visiwa vya Unguja na Pemba ilitangaza uhuru wake tarehe 12 January, mwaka wa 1964 baada ya mapinduzi yaliyomwaga damu yaliyomaliza karne kadhaa za utawala wa kisultani wa Waarabu.

Baada ya miezi mitatu Zanzibar ilijiunga na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ikabaki na utawala wa kijimbo, rais, katiba na bendera yake.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mapema miaka ya tisini, visiwa hivyo vimekuwa vikishuhudia mapambano makali kati ya chama tawala CCM na chama kikuu cha upinzani cha CUF, haswa wakati wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment