KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 5, 2010

Mtikila huru, aponyeka kuingia gerezani

MAHAKAMA ya Wilaya ya IIala, imemuachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, baada ya kulipa deni lililokuwa likimkabili la shilingi Milioni 9.8 kutoka kwa Bi. Paskazia Matete.
Mtikila amelipa deni hilo kufuatia kuonja joto ya jiwe baada ya kuwekwa ndani kwa siku moja katika kituo cha polisi cha Msimbazi kilichopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

AWali Mahakama hiyo ilimuhukumu mchungaji huyo kwenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela baada ya mchungaji huyo kushindwa kulipa deni hilo na mahakama ilisikiliza ombi la mlalamikaji na kutoa hukumu hiyo. Wakati hukumu hiyo inatolewa mchungaji huyo hakuwepo mahakamani.

Jana Mtikila alilipa deni hilo mbele ya hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bi. Joyce Minde na alilipa deni la sh.9,869,000 lililokuwa likimkabili kwa mdai wake.

Hivyo mahakama hiyo imefuta hukumu ambayo awali iliitoa dhidi ya mshitakiwa huyo na hakimu kusema rufaa ipo wazi kwa yeyote ambaye ataona hakuridhishwa basi atakata rufaa.

Mara baada ya kutoka nje ya mahakama Mtikila alidai atakata rufaa kwa kuwa aliona kuna uonevu dhidi yake na kudai mlalamikaji anatumiwa na maadui zake ili aweze kumchafua jina.

No comments:

Post a Comment