KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 5, 2010

Naomi Campell alipewa 'mawe machafu'

Naomi Campell alipewa 'mawe machafu'
Mwanamitindo Naomi Campbell amesema alipewa "mawe machafu" baada ya chakula cha jioni ambacho kiongozi huyo wa zamani wa Liberia alikuwepo. Baadaye Bi. Campbell aliambiwa mawe hayo huenda ni almasi.


Naomi Campbell akitoa ushahidi


Bi. Campbell alikuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Charles Taylor kuhusu tuhuma kuwa rais huyo wa zamani alimpa Campbell "almasi zenye damu" kama zawadi mwaka 1997.

Kesi hiyo inaendeshwa mjini The Hague, nchini Uholanzi, katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.


Charles taylor anakanusha mashitaka

Waendesha mashitaka wamesema ushahidi wake unaweza kumhusisha Bw. Taylor na madini hayo, ambayo yanatuhumiwa kutumika kufadhili vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

Bw. Taylor anakanusha mashitaka hayo.

Amesema hakuwahi kuuza ama kufanya biashara ya almasi ili kupata silaha.

Zawadi yako

Bi. Campbell , aliapa kwa kutumia Biblia kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.


Naomi Campbell akila kiapo kabla ya kutoa ushahidi


Bi. Campbell amesema alipewa vipande viwili au vitatu vya madini yasiyokatwa, baada ya chakula cha jioni nchini Afrika Kusini. Hafla hiyo ya watu maarufu iliandaliwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, na ilihudhuriwa na mcheza sinema wa Marekani Mia Farrow pamoja na wengine, akiwemo Bw. Taylor.

Kabla ya kukutana na Bw. Taylor, Bi Campbell amesema alikuwa hajawahi kumsikia rais huyo wala nchi ya Liberia. Amesema wakati amelala chumbani kwake usiku alisikia mlango wa chumba chake ukigongwa. "Nilipofungua mlango nilikutana na watu wawili walionipa kifuko kidogo na kusema 'zawadi yako'," amesema Bi. Campbell.

Amesema watu hao wawili hawakujitambulisha wao ni nani. Amesema alikiweka kifuko hicho karibu na kitanda chake bila kuangalia kuna nini ndani, na kuendelea kulala. "Nilikifungua kifuko hicho asubuhi nilipoamka na kuona mawe kadhaa, yalikuwa madogo na yakionekana kama machafu" ameiambia Mahakama.

Hakukuwa na maelezo yoyote, ameongeza. "Asubuhi wakati wa chai nilimwambia Bi. Farrow pamoja na Carol White [mwakilishi wa Campbell wa zamani] kilichotokea usiku na mmoja kati yao akasema 'Huyo lazima atakuwa Charles Taylor', na mimi nikasema 'huenda ni yeye'."


Kupokea almasi

Naomi CampbellAlizaliwa London, Uingereza mwaka 1970 na wazazi wenye asili ya Carribean na Uchina
Ni mmoja wa wanamitindo wanaolipwa fedha nyingi, baada ya kipaji chake kuonekana akiwa tangu shule
Picha yake ilitoka katika ukurasa wa mbele wa gazeti la Elle akiwa na miaka 15
Ametangaza nguo za watengenezaji wenye sifa na pia kuanzisha manukato yake mwenyewe
Mwaka 2008, alihukumiwa kufanya huduma kwa jamii kwa saa 200 nchini Uingereza baada ya kuwashambulia maafisa wawili wa polisi ndani ya ndege kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow
Mwaka 2009, alimaliza kesi nje ya mahakama dhidi ya mfanyakazi wake aliyekuwa akidai kuwa mwanamitindo huyo alimshambulia. Bi Campbell alikanusha madai hayo.
Amesema wakati huo, hakuwa anafahamu lolote kuhusu sheria ya umiliki wa almasi zisizokatwa. Amesema alimpa mawe hayo Jeremy Ratcliffe, ambaye ni mwakilishi wa wakfu wa watoto wa Nelson Mandela, kwa sababu alitaka mawe hayo yatolewe kwa ajili ya kusaidia watu, na kusema alipozungumza na Bw. Ratcliffe kwa simu mwaka 2009, bado alikuwa nayo.

Katika barua iliyowasilishwa katika mahakama na upande wa utetezi, wakfu wa watoto wa Nelson Mandela umesema "Haujawahi kupokea almasi kutoka kwa Bi. Campbell au kutoka kwa mtu yeyote yule. Isingekuwa sahihi na kinyume cha sheria kufanya hivyo."

Bi. Campbell amemwambia wakili wa upande wa utetezi Coutenay Griffiths kuwa hakukaa karibu na Bw. Taylor wakati wa hafla ya chakula cha jioni, tofauti na maelezo yaliyotolewa na mwakilishi wake wa zamani Carol White.

Katika taarifa yake kwa mahakama, Bi. White alisema Bi. Campbell na Bw. Taylor walikuwa wakitupiana macho na kufanya mzaha wakati wote wa chakula.

Kusema uongo


Naomi Campbell

Bw. Griffiths amesema "Shahidi [Bi. White] alimsikia Bw. Taylor akimwambia Bi. Campbell kuwa atamtumia almasi. Taylor na watu wake walikuwa wanakaa mbali kidogo, kwa hiyo mipango ilifanywa ya kutuma watu kumpelekea zawadi hiyo. Je ni kweli au uongo?."

"Hiyo si kweli kabisa," alijibu Bi. Campbell.

Bw. Griffiths amesema Bi. White alisema Bi. Campbell alifurahishwa na wazo hilo la kupatiwa almasi na Bw. Taylor, lakini Bi. Campbell amekanusha jambo hilo.

Bi. White na Bi. Campbell kwa sasa wanavutana katika mzozo wa kisheria, amesema Bw. Griffiths. "Huyu ni mwanamke mwenye sababu ya kusema uongo dhidi yako?" aliuliza. "Haswa," alijibu Bi. Campbell.

Sikutaka kuwa hapa. Nimetakiwa kuwa hapa... hii imeathiri shughuli zangu
Bi. Naomi Campbell

Mwendesha mashitaka amesema Bi. Campbell alikuwa akijibu swali, kabla swali halijamalizika kuulizwa, na kuuliza iwapo ana wasiwasi. "Hapana, naam, sikutaka kuwa hapa. Nimetakiwa kuwa hapa," alijibu Bi. Campbell. "Kwa hiyo kwa hakika nataka nimalizane na hili, ili niendelee na maisha yangu ya kawaida. Hii imeathiri shughuli zangu"

Amesema aliwahi kukanusha kuwahi kuwa na mawe hayo kwa kuwa alikuwa na wasiwasi wa yatakayoweza kuikuta familia yake kwa sababu Bw. Taylor alikuwa 'mtu anayedaiwa kuuwa maelfu ya watu, kama nilivyosoma kwenye mtandao'.

Majeshi ya waasi


Tuhuma za madini hayo yasiyokatwa kupewa Bi. Campbell zilijitokeza katika maelezo yaliyotolewa na Mia Farrow.

'Almasi zenye damu' ni madini yanayochimbwa katika maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya waasi, na hutumika kufadhili ghasia.

Bi Campbell alikuwa shahidi asiyetaka kujitokeza, na aliamriwa na upande wa mashitaka kufika mahakamani, la sivyo angekabiliwa na mashitaka mengine ya kisheria.

Mwezi Aprili, Bi. Campbell alikiambia kituo cha televisheni cha ABC cha Marekani kuwa "hajawahi kupokea almasi" kutoka kwa Bw. Taylor, na kuwa hakutaka kuzungumzia suala hilo.


Naomi Campbell

Baadaye, alikiambia kipindi cha Oprah Winfrey cha Marekani, kuwa hakutaka kuhusika katika kesi ya Bw. Taylor na kuwa anahofia maisha yake, iwapo atafanya hivyo.

Hata hivyo, kampuni inayomdhamini baadaye ilitoa taarifa inayothibitisha kuwa, Bi. Campbell atahudhuria mahakama hiyo "kuweka sawa matukio ya mwaka 1997".

Bi. Campbell amepata amri ya mahakama inayozuia picha zake kuonesha akiwa nje ya mahakama, ingawa taratibu za ndani ya mahakama zimeonesha kupitia televisheni.

Bw. Taylor, mwenye umri wa miaka 62, anashukiwa kuuza almasi ili kununua silaha kwa ajili ya waasi wa RUF wa Sierra Leone, ambao walifahamika kwa kukata mikono na miguu ya raia wa nchi hiyo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1991 hadi 2001.

Kuongoza waasi

Kesi hiyo imefikia hatua ya utetezi, huku mashahidi wachache wakisalia kutoa ushahidi.

Upande wa mashitaka ulimaliza kuhoji mashahidi mwezi Februari mwaka 2009, baada ya kuita mashahidi 91, lakini hata hivyo walipata kibali maalum cha kufungua upya kesi yao ili kuwasilisha ushahidi mpya.

Waendehsha mashitaka wamesema katika nafasi yake nchini Liberia, Bw. Taylor pia aliwapa mafunzo na kuongoza waasi hao.

Alikamatwa mwaka 2006, na kesi yake kufunguliwa mwaka 2007.

Bw. Taylor alikanusha mashitaka 11, likiwemo shitaka la uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadam, katika mahakama hiyo inayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa.

Maelfu ya watu walikufa katika machafuko ya nchi za Sierra Leone na Liberia.

No comments:

Post a Comment