KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, July 10, 2010

Wapenzi wa jinsia moja hawateswi Cameroon


Serikali ya Cameroon imekana madai ya mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja anayetafuta hifadhi Uingereza kuwa atateswa iwapo atarudi kwao.

Siku ya Jumatano, mahakama kuu ya London ilimkubalia mtu huyo kubaki Uingereza pamoja na mwengine kutoka Iran.

Adhabu inayotolewa kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Cameroon ni hadi miaka mitatu jela.

Hata hivyo, waziri wa mawasiliano wa Cameroon ameiambia BBC kuwa watu hao wanaruhusiwa kufanya vyovyote kwa faragha bila kubughudhiwa na yeyote.

Waziri wa mawasiliano Issa Tchiroma amesema, " Mapenzi ya jinsia moja yanakatazwa kwa mujibu wa sheria, hilo halina shaka. Lakini naweza kusisitiza kwamba hakuna hata mmoja aliyefanya mapenzi hayo akateswa hapa Cameroon."

Ameiambia BBC kwamba mtu huyo ametumia tu sheria hiyo ili aweze kupata hifadhi Uingereza.

"Unadhani yeye ndiye mtu peke anayefanya mapenzi ya jinsia moja Cameroon."
'Watu wenye hasira'

Watu hao wawili ambao sasa wameshinda kesi na kupata hifadhi ya kubaki Uingereza walikataliwa ombi lao hilo na serikali iliyopita ya Uingereza.

Uamuzi huo uliungwa mkono na mahakama ndogo, kwa minajili ya kwamba wanaweza kuepuka kuteswa iwapo wataficha jinsia yao au kufanya mapenzi hayo kwa siri.

Lakini mahakama kuu imeamua kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Mtu huyo kutoka Cameroon, ambaye anatambuliwa tu kama HT, aliambiwa ahame eneo jingine nchini humo na afanye shughuli zake kwa siri.

Alishambuliwa na watu wenye hasira huko nyumbani baada ya kuonekana akimbusu mwenzake. Amekuwa akihangaika kubaki Uingereza katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Awali HT aliiambia BBC, "Watu wengine walinisimamisha na kusema "tunajua wewe unashiriki mapenzi ya jinsia moja'.

" Siwezi kurudi na kujificha au kudanganya kuhusu jinsia yangu. Nikirudi nyumbani nitaishi kwa hofu."

HT na mwenzake kutoka Iran, nchi ambayo hutoa adhabu ya kifo kwa wapenzi wa jinsia moja, sasa kesi zao zitapitiwa na mahakama za uhamiaji.

Mwandishi wa BBC Randy Joe Sa'ah huko Cameroon amesema mbali na mawakili wachache na mwimbaji maarufu wa nchi hiyo Petit Pays, hakuna makundi yeyote yanayotetea haki za watu wa jinsia moja nchini humo.

No comments:

Post a Comment