KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Sunday, July 11, 2010

Ujerumani yatwaa nafasi ya tatu

Ujerumani imenyakua nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, baada ya kuifunga Uruguay mabao 3-2 katika uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port Elizabeth.

Sami Khedira aliifungia Ujerumani bao la ushindi katika dakika ya 82 baada ya ngome ya ulinzi ya Uruguay kushindwa kuondosha mpira wa kona uliopigwa na Mesut Ozil.
Sekunde chache kabla ya mchuano kumalizika mshambuliaji wa Uruguay Diego Forlan alipiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba.
Ujerumani ndio waliotangulia kufunga katika dakika ya 18 kupitia Thomas Muller, kabla ya Edinson Cavani kuisawazishia Uruguay dakika 10 baadaye.
Lala salama

Kipindi cha kwanza kilimalizika 1-1 na dakika 6 baada ya cha pili kuanza Diego Forlan alisukumiza wavuni pasi kutoka kwa Egidio Arevalo, Uruguay ikawa inaongoza 2-1.
Hilo lilikuwa bao la tano la Forlan kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia, na ni miongoni mwa wafungaji bora.
Katika dakika ya 56, Marcell Jansen aliisawazishia Ujerumani kwa bao la kichwa baada ya krosi ya Jerome Boateng kumzidi mlinda mlango Fernando Muslera.

Baada ya Sami Khedira kuifungia Ujerumani bao la ushindi , Uruguay walizidisha mashambulizi bila mafanikio.

Kocha wa Ujerumani, Joachim Loew, aliwapumzisha wachezaji mashuhuri miongoni mwao mshambuliaji Miroslav Klose, Likas Podolsi na mlinzi Philip Lahm.


Klose alikosa nafasi ya kufikisha goli la 15 idadi ambayo mshambuliaji wa Brazil, Ronaldo amekwisha funga katika historia ya mashindano ya Kombe la Dunia

No comments:

Post a Comment