KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 23, 2010

Mradi wa dhahabu kuanzishwa Congo


Kampuni ya uchimbaji madini ya Randgold, imesema itaanzisha mradi mkubwa zaidi barani Afrika wa uchimbaji madini ya dhahabu mashariki mwa Congo.

Mradi huo utasababisha watu 15,000 kuhamishwa kutoka makaazi yao, lakini kampuni ya Randgold inasema mradi huo unaungwa mkono na serikali na watu wanaoishi katika eneo hilo.

Mgodi huo wa madini unaaminika kuwa na tani 320 za dhahabu. Ni mkubwa kama migodi ya Afrika Kusini ambayo ni kati ya nchi ambazo huzalisha kiwango cha juu zaidi cha dhahabu duniani.


Wachimbaji madini
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ina utajiri mkubwa wa madini lakini idadi kubwa ya watu huishi katika hali ya umaskini.

Kampuni ya Randgold, ambayo inatambulika katika soko la hisa la London, inasema itaanzisha mradi huo wa uchimbaji madini katikati mwa mwaka 2011.

Mradi huo utajulikana kama Kibali, na uko katika eneo la jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo linalopakana na Uganda.

Ili kuanza mradi huo, kampuni ya Randgold itajenga barabara ya kilomita 180 itakayoelekea Uganda.

Mradi huo wa Kibali uko karibu na eneo ambalo ni ngome ya kundi la wapiganaji la LRA kutoka Uganda, lakini kampuni hiyo inasema maafisa wa usalama wamewahakikishia kuwa mradi huo unaweza kuendelea bila tatizo.

Mkuu wa kampuni hiyo Mark Bristow, amesema mradi huo utakuwa salama. Amesema wakaazi wa eneo hilo watahamishwa na kupelekwa katika kijiji kipya kilichojengwa na kampuni hiyo.

No comments:

Post a Comment