KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 23, 2010

Askofu Desmond Tutu kustaafu shughuli za umma


Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana Desmond Tutu ametangaza kustaafu kwake kutoka shughuli za umma.

Mshindi huyo wa tuzo ya Nobel alikuwa mtetezi mkuu wa haki za binadamu na alipinga utawala wa ubaguzi wa rangi Aparthied nchini Afrika Kusini .

Desmond Tutu ametaja kilele cha kazi yake, kuwa siku aliyomtangaza Nelson Mandela kama rais wa kwanza wa Afrika Kusini aliyechaguliwa kidemokrasia, mwaka wa tisini na nne.

Aliwaambia wanahabari kuwa ananuia kupumzika na familia yake akitimia miaka sabini na tisa mwezi Oktoba mwaka huu.

Miaka michache kabla Nelson Mandela aachiwe huru, wakati harakati za ukombozi kutoka utawala wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini zili shika kasi, Askofu Desmond Tutu alikuwa mstari wa mbele.

Wakati wa maandamano ya kupinga serikali hiyo dhalimu, alijitokeza na vazi lake rasmi akiongoza waandamanaji. Mara kadhaa vurugu zilizuka na aliweka maisha yake hatarini akijaribu kutuliza pande zote mbili, hapo ikiwa ni vikosi vya usalama na wandamanaji waliokuwa na jazba mno. Na sio wakati wote alifaulu au hata kusikizwa.

Mara kadhaa askofu huyo kwa kanisa la Kianglikana aliikemea serikali na kuikumbusha kuwa sera zake zilikuwa zinakiuka upendo wa Mungu ndio maana akapewa jina la askofu wa wanasiasa. Ni juhudi hizo ambazo zilichangia yeye kupewa tuzo ya amani ya Nobel mwaka wa 84. Na kwa heshima hiyo Rais Nelson Mandela alimpa jukumu la kuongoza Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini mwaka wa 95.

Ingawa harakati za ukombozi na ujenzi wa taifa mpya la Afrika Kusini ndizo zilizochukua wakati wake mwingi, hakusita kukosoa viongozi wengine duniani walioonekana kuwadhulumu raia wao.

Maarufu kabisa ni msimamo wake kuhusu siasa za Zimbabwe. Rais Robert Mugabe alichukizwa sana na kauli zake na hata wakati mmoja kumuita, "Askofu mfupi mwenye hasira na chuki."

Lakini licha ya hilo, Askofu Tutu anapendwa sana, alizaliwa mjini Transvaal na kipindi fulani alikuwa mwalimu lakini pale serikali ilipoanzisha sera ya kubagua wanafunzi aliamua kuwa kasisi.

Mwaka wa 75 alisimikwa kama Dean wakwanza mwafrika wa kanisa la Kianglikana mjini Johannesburg na hatimae kuwa askofu wa kwanza mwafrika mwaka wa 86 alipoteuliwa kuwa Askofu wa kanisa hilo mjini Cape Town.

Kumbukumbu ya wengi kumhusu itakuwa mapema mwezi huu, alipokuwa kwenye sherehe ya uzinduzi wa kombe la dunia ambapo alionekana kuwa na furaha kupita kiasi kila mara akicheza dansi.

Lakini kwake Askofu Desmond Tutu, kumtambulisha Nelson Mandela kama rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini ndio sabuni ya moyo wake.

No comments:

Post a Comment