KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 23, 2010

Mkutano wa afya kampala wapoteza mada


Viongozi wa mataifa ya Muungano wa Afrika AU watakutana mjini Kampala mwishoni mwa wiki hii kujadili masuala ya afya ya jamii kwa kina mama na watoto.

Hata hivyo, baadhi ya wahusika wanahofia kuwa mada ya mkutano huo huenda ikapuuzwa na badala yake masuala ya usalama yakapewa kipaumbele.

Katika vikao mbali mbali, tangu kuanza kwa mkutano huo siku ya Jumatatu, swala lililotawala mijadala ni usalama na mgogoro wa Somalia.

Waziri wa mambo ya nje wa Uganda, Henry Oryem Okello, amesema kuwa licha ya kuwa mkutano ulilenga kujadili suala la afya ya uzazi kati ya mama na mtoto inasikitisha kuona kuwa migogoro ya Somalia imepiku mada ya afya.

" Tangu tuanze kukutana, watu wote wanazungumzia namna serikali za Afrika zinaweza kusaidia kuwapiga na kuwafukuza magaidi wanaotatiza usalama nchini Somalia" alisema Bw Okello.

Malalamiko

Wadadisi wanasema kuwa huenda hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa migogoro barani Afrika. Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, ambaye pia anahudhuria mkutano huo, Bw Mohammed Maundi, alisema hatua hiyo inaonyesha matumaini ya waafrika kuimarisha usalama barani.

"Afrika imejizatiti kutambua kuwa migogoro ni yetu, na pia imejitolea kutafuta ufumbuzi kwa masuala hayo. Na ndiyo maana katika Muungano wa Afrika - AU, tunaweka taasisi za kushughulikia masuala haya."

Hata hivyo baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa hicho ni kisingizio cha wanaume kukwepa kuzungumzia suala nyeti linalowahusu wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment