KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, July 13, 2010

Milipuko 'yaua watu 23' Uganda

Takriban watu 23 wameuawa katika milipuko miwili iliotokea kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Haijajulikana mpaka sasa milipuko hiyo imesababishwa na nini, ambapo polisi wamesema imelipuka katika klabu ya mchezo wa raga na kwenye mgahawa, wakati mashabiki walipokuwa wakitazama Kombe la Dunia.

Inspekta wa Polisi Kal Kayihura ameliambia shirika la habari la AFP, “ Kwa hakika mabomu haya yalikuwa yakilenga watu waliokusanyika kuangalia Kombe la Dunia.”

Wanamgambo wa Kisomali hapo awali waliwahi kutishia kushambulia mji wa Kampala; majeshi ya Uganda yapo mjini Mogadishu kulinda amani.

Bw Kayihura ameliambia shirika la habari la AP kwamba anaamini kundi la wanamgambo la al-Shabab linahusika na shambulio hilo.

Baada ya tukio moja miongoni mwa milipuko hiyo Bw Kayihura alisema, “ Taarifa tulizonazo zinaonyesha kwamba watu 13 wamekufa hapa katika mgahawa wa Ethiopian village na wengine wengi wamejeruhiwa na zaidi ya 10 wameripotiwa kufariki dunia katika klabu ya raga.”

Takriban majeshi 5,000 ya Afrika ya kutunza amani kutoka Uganda na Burundi yapo kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kuilinda serikali ya mpito iliyopo.

Jeshi hilo la Amisom limejikuta kwenye mapigano na wanamgambo wanaodhibiti eneo kubwa la Somalia ya kati na kusini.

No comments:

Post a Comment