KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 30, 2010

Maafisa Afya kizimbani kwa kupokea rushwa


MAAFISA Afya Wilaya ya Kinondoni wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya kiasi cha shilingi laki moja kutoka kwa muuza duka.
Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani jana kusomewa maelezo ya awali ni Ezra Gula (28) na Gelma Chifunda (39) ambao wote ni waajiriwa wa Serikali kitengo cha afisa afya Wilaya ya Kinondoni.

Watuhumiwa ambao wote ni wakazi wa Mbezi walikamatwa Julai 21 na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kuwekewa mtego.

Wakisomewa maelezo ya awali na Mwanasheria wa TAKUKURU mkoa wa Kinondoni Ronald Manyiri alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Julai 21 huko Mwananyamala Kinondoni.

Watuhumiwa walikiuka majukumu yao kwa kuomba hongo, baada ya kufanya ukaguzi wa duka la Simon Shilayo ambapo walipokagua walibaini baadhi ya bidhaa zilikuwa zimekwisha muda wake (zimeexpire).

Watuhumiwa walimtaka Shilayo awape kiasi cha shilingi laki moja ili wasimchukulie hatua hata hivyo baada ya kukubaliana muuza duka huyo aliweka mitego ya TAKUKURU na kufanikiwa kuwakamata.

Watuhumiwa hao walikana kosa hilo ambapo waliachiwa kwa dhamana ya shilingi laki mbili kila mmoja pamoja na wadhamini wawili wawili ambapo kesi imeahirishwa hadi Agosti 16 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment