KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, June 8, 2010

Vifo zaidi vya sumu vyahofiwa Nigeria


Mtaalamu wa kuondosha uchafu amesema, mamia ya watoto wengine huenda wakafariki dunia kaskazini mwa Nigeria.

Mashine nzito zinatarajiwa kutumika kuondosha udongo katika kijiji kimoja nchini Nigeria ambapo takriban watoto 100 wamefariki dunia kutokana na kinachodhaniwa kuwa ni sumu ya risasi.

Maafisa wanasema udongo wa juu wa sentimeta 5 katika kijiji cha Yar'Gailma kaskazini mwa nchi hiyo utachimbuliwa.

Watoto 25 kutoka kijiji hicho wamelazwa hospitali na wengine 80 wakitarajiwa kupewa matibabu katika siku zijazo.

Takriban watu 163 wamefariki dunia eneo hilo baada ya wakazi kuanza kuchimba dhahabu kwenye maeneo yenye kiwango kikubwa cha sumu hiyo.

Mamlaka ya afya yameunda kambi mbili katika jimbo la Zamfara kuwatibu watu wenye dalili za kudhurika na sumu hiyo.

Mwandishi wa BBC katika jimbo la Zamfara, Haruna Shehu Tangaza amesema nyumba eneo hilo hazitobomolewa - sakafu zinatarajiwa kufunikwa na saruji ili kuwalinda wakaazi kutokana na sumu hiyo ya risasi.

Wasiwasi wa majira ya mvua
Vifo hivyo viligunduliwa wakati wa mpango wa kinga unaofanyika kila mwaka, maafisa walipotambua kulikuwa hakuna watoto katika vijiji kadhaa.

Wanakijiji walisema watoto hao walikufa kwa malaria na ni mpaka wafanyakazi kutoka shirika la kimataifa la kutoa msaada Medecins Sans Frontiers walipowapima damu wakaazi hao na kugundua walikuwa na kiwango kikubwa cha sumu hiyo.

Mwandishi wetu amesema, hivi karibuni jimbo la Zamfara liliajiri kampuni ya China kwa ajili ya kuchimba dhahabu eneo hilo.

Lakini wanakijiji nao walijaribu kugeuza mtaji kwa kuchimba madini hayo yenye thamani - jambo lililo kinyume na sheria huko Nigeria.

Waandishi wamesema, watu hao walianza kuumwa baada ya sumu hiyo iliyotolewa wakati wa kusafisha mawe yenye madini ya dhahabu yalipochafua mfumo wa maji eneo hilo.

Baadhi wanahofia kuwa uchafuzi huo unaweza kuenea wakati wa msimu wa mvua ambao ndio kwanza umeanza.

No comments:

Post a Comment