Maafisa wa afya wamesema zaidi ya watoto mia moja wamefariki dunia kutokana na sumu ya madini ya risasi nchini Nigeria katika majuma ya hivi karibuni.
Idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka tangu mwezi March, baada ya wakaazi kuanza kuchimba dhahabu kinyume cha sheria katika maeneo yenye madini mengi ya risasi au lead.
Wengi wa waathiriwa ni kutoka maeneo ya vijijini katika jimbo la Zamfara, kaskazini mwa nchi.
Jumla ya kesi 163 kati ya kesi 355 zimesababisha vifo, kulingana na afisa wa afya kutoka Nigeria.
Dr Henry Akpan, afisa katika wizara ya afya, alisema " waathiriwa walikuwa wakichimba dhahabu, lakini maeneo hayo yana kiwango kikubwa cha sumu ya madini ya risasi".
Maafisa wa afya wameweka kambi mbili katika eneo hilo kuwatibu watu wanaosumbuliwa na dalili za sumu hiyo ya madini ya risasi.
Mwandishi wa BBC mjini Kaduna amesema vifo hivyo viligunduliwa wakati wa chanjo ya kila mwaka inayofanyika nchini, baada ya maafisa kutambua kuwa hakuna watoto katika maeneo ya vijijini ya jimbo hilo la kaskazini mwa nchi.
Wanavijiji walisema kuwa watoto walikufa kwa ugonjwa wa malaria, lakini baada ya kundi la madaktari kutoka shirika la kimataifa la Medecins Sans Frontiers kufanya vipimo vya damu wakagundua kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sumu hiyo.
Jimbo la Zamfara hivi karibuni liliipatia kandarasi kampuni kutoka Uchina kuchimba dhahabu katika eneo hilo.
Lakini wanavijiji nao walijaribu kujinufaisha kwa kuchimba dhahabu bila ya idhini, jambo ambalo ni kosa nchini Nigeria.
Mwandishi wa BBC anasema huenda wakaazi hao waligonjeka baada ya sumu iliyotokana na mfumo wa kusafisha dhahabu hiyo kuchanganyika na maji.
No comments:
Post a Comment