Rafa Benitez mbioni kuondoka Liverpool
Utawala wa Rafa Benitez katika timu ya Liverpool umefikia kikomo baada ya timu hiyo kubwa ya ligi kuu ya soka ya England kutangaza kuwa ameondoka baada ya kufikia makubaliano ya muafaka.
Benitez mwenye umri wa miaka 50, anaondoka Liverpool baada ya miaka sita. Ingawa bado haijajulikana nani anaandaliwa kumrithi kocha huyo, pia Benitez hajasema kama atahamia timu nyingine.
Benitez atalipwa fungu la mamilioni ya pauni kama fidia kuondoka Anfield.
Kocha huyo kutoka Hispania, mwenye umri wa miaka 50, alisaini mkataba wa miaka mitano Machi 2009, lakini alishindwa kupata mafanikio msimu uliopita hasa baada ya timu yake kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya.
Wasi wasi
Liverpool wana madeni ya pauni milioni 351 na wamiliki wake Tom Hicks na George Gillett mapema mwaka huu walitangaza nia ya kutaka kuiuza.
Umiliki wa Liverpool kwa raia hao wawili wa Marekani umezua malalamiko kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo, ambao hawajafurahishwa na uendeshaji wake.
Habari za kuondoka kwa Benitez zitasababisha wasi wasi kuhusu hatma ya baadhi ya wachezaji muhimu.
Nahodha Steven Gerrard, mshambuliaji nyota Fernando Torres na kiungo Javier Mascherano wametajwa kuwaniwa na timu nyingine baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment