Chuo cha kwa kwanza kabisa nchini cha masuala ya urembo kiitwacho Pure Academy kimezinduliwa jijini Dar es Salaam na kozi zitaanza mwezi wa nane mwaka huu.
Muasisi wake Yasmin Shariff kutoka Canada alisema chuo hicho cha aina yake ni cha kwanza hapa nchini na kwamba ana matumaini kitasaidia kutengeneza ajira nyingi kwa wasichana na wavulana hapa nchini.
Shule hiyo imezinduliwa katika hoteli ya Double Tree iliyopo maeneo ya Msasani Slip Way jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Masuala ya Jinsia katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Winifrida Rutahindurwa.
Rutahindurwa alisema Chuo hicho kitakapoanza kazi kitawasaidia vijana wengi wa Kitanzania kupata ajira pamoja na kuifanya taaluma ya Urembo kuwa yenye heshima katika jamii.
“Kwa kweli ninawapongeza sana kwa kuanzisha Chuo hiki na ni matumaini yangu kwamba kitasaidia sana katika kutengeneza ajira kwa vijana, hongereni sana”
Naye mwasisi wa chuo hicho Yasmin alisema chuo hicho ni chuo cha aina yake hapa nchini na ni cha kwanza kuzinduliwa ,kitatoa elimu ya urembo, mfano mitindo ya nywele, kupaka vipodozi na kutunza ngozi na masuala mengine yanayohusu urembo na kwamba kipo wazi kwa vijana wote wa jinsia zote.
Chuo cha Pure kinatambua kwamba mvuto katika urembo na mitindo ni muhimu sana katika jamii yetu, ndiyo maana tumeleta chuo ambacho kitainyanyua taaluma ya urembo hapa nchini.
Mbali na Chuo hicho, pia wataanzisha Saluni ya kisasa hapa nchini ambayo itakuwa katika kiwango cha kimataifa.
“ Matarajio yangu ni makubwa, licha ya kuwa na shule ya kisasa pia ningependa kufungua saluni ya kike ambayo itakuwa katika kiwango cha kimataifa,” alisema.
Wanafunzi wataweza kupata elimu yenye kiwango cha kimataifa kwa ada ya kiwango cha chini kabisa ambayo kila mmoja ataweza kuimudu ukilinganisha na kwenda nchi za nje ya nchi kupata elimu.
“Tumeleta walimu wataalamu na waliobobea katika fani hii kutoka Canada na Marekani waliobobea na wenye uzoefu wa kimataifa tumewatengenezea wanafunzi mazingira ya kufanya kazi kimataifa.”
Alisema wazo la kuwaleta wataalamu wa kimataifa ni kutengeneza uelewa mkubwa wenye kiwango cha kimataifa na hii itawapa wanafunzi mwanga mkubwa katika biashara ya urembo na uelewa mkubwa katika kujifunza.
No comments:
Post a Comment