KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

Waziri Mkulo asimchanganye Kaizari na Mungu - Maaskofu

SAKATA LA MISAMAHA YA KODI

:: Wasema serikali inao uwezo wa kubaini wafujaji
:: Wasikitishwa kwa kutohusishwa mapema
:: Serikali yawalainisha kwa kutoa ufafanuzi

Na Julian Msacky

WAKATI leo Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo anatarajiwa kufunga mjadala kuhusu bajeti ya serikali ya mwaka 2009/2010, sababu zilizosababisha mvutano kati ya taasisi za dini na serikali zimebainika.

Moja ya sababu hizo ni kitendo cha serikali kuandaa bajeti yake na kuweka kipengele kinachotazana upya misamaha ya kodi kwa asasi za kiraia na taasisi za dini bila kuzihusisha taasisi hizo.

Kitendo hiki, kinafafanuliwa na viongozi wa dini kama mbinu mpya ya serikali kutobaini umuhimu wa taasisi za dini katika maendeleo ya nchi na pia kinabainisha kuwapo hali tata kati ya taasisi hizi na serikali.

Serikali kwa upande wake inasisitiza kuwa, imefikia hatua hiyo kutokana na kuwapo msukosuko wa kiuchumi ambao umeathiri taifa. Ni kutokana na hali hiyo na serikali imejitathmini upya na kubaini kuna maeneo ambayo yamekuwa yakilifanya taifa kukosa mapato.

Eneo mojawapo linalozungumzwa ni lile la msamaha wa kodi uliokuwa ukitolewa kwa asasi zisizo za serikali na taasisi za dini ambayo sasa imefutwa.

Kufutwa kwa misamaha hiyo kunaelezwa ni kutokana na kuwapo mianya tata katika uagizaji wa vifaa mbalimbali vya asasi zisizo za serikali sambamba na taasisi za dini.

Waziri Mkulo anafafanua kuwa; “Kuna taasisi moja ya dini ilipotaka msamaha wa VAT kwa matairi ya magari zaidi ya 400, lakini uchunguzi ulipofanyika ilibainika kuwa taasisi hiyo ina magari yasiyozidi matano.

“Taasisi nyingine ilipochukua msamaha wa VAT kwa mabati 4,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya ibada, lakini uchunguzi ulipofanyika iligundulika kwamba ujenzi wa nyumba ulihitaji mabati 200,” alisema Mkulo.

Wakati Waziri Mkulo akisema hivyo; Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini anafafanua kuwa, mifano inayotolewa na Mkulo inaonyesha ubabaishaji na hailengi kutafuta chanzo cha tatizo na suluhisho lake.

Askofu Kilaini aliliambia gazeti hili juzi kuwa, serikali ndiyo inayosajili taasisi za dini na asasi zisizo za serikali na ina jukumu la kuzichukulia hatua zile ambazo zinatumia vibaya misaada inayosamehewa kodi.

Askofu Kilaini anafafanua kuwa: “Siku hizi kuna taasisi za dini ambazo zimeibuka kwa ajili kutafuta fedha. Kwa sababu serikali ndiyo inazipatia taasisi za kidini usajili na pia misamaha hiyo ya kodi ni wajibu wa serikali yenyewe kuzibaini kama zinakwenda kinyume na msamahaka huo.”

Askofu Kilaini anaeleza kuwa, kabla ya serikali kufikia uamuzi wa kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini, ilipaswa kubaini umuhimu wa taasisi hizo hasa katika maendeleo ya sekta za elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.

“Kuziondolea msamaha wa kodi taasisi hizi, kutaumiza wananchi wanaopata huduma kwa sababu gharama zake zitakuwa juu. Hii ni wazi itawaathiri wananchi moja kwa moja,” anahitimisha Kilaini.

Kwa upande wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Volentino Mokiwa yeye aliliambia Rai kuwa, kama kweli kuna madai ya kutumia misaada wanayopata mashirika ya dini baada ya kusamehewa kodi basi huo ni uhuni.

“Kama kweli kuna viongozi wa aina hii, na hata kama mimi ni mmojawapo basi niko tayari nitajwe na serikali,” anasema Askofu Mokiwa.

Kama ilivyokuwa kwa Askofu Kilaini, Askofu Mokiwa pia alifafanua kuwa, tamko la serikali kupitia kwa waziri Mkulo kwamba zipo taasisi zinazotumia vibaya misamaha ya kodi linaonyesha ubabaishaji wa serikali katika kutumia nafasi za madaraka yake.

“Kama suala lipo maana yake ni kwamba, serikali yenyewe ina tatizo. Ilitakiwa ishughulike mapema na hizo taasisi inazodai zinatumia vibaya misamaha hiyo,” na kuongeza kwamba; “ni wakati muafaka iwataje wahusika.”

Askofu Mokiwa alifafanua pia kuwa, kinachoonekana kwa sasa serikali ndio inayolea tatizo hilo kwa sababu ina uwezo wa kuliondoa. Kutokana na hali hiyo, Askofu huyo alisema, inachotakiwa kufanya ni serikali kuhakikisha “Cha Kaizari anapewa Kaisari na cha Mungu anapewe Mungu”.

Baada ya viongozi wa dini kulalamikia mno suala hilo, Mkulo alikutana na waandishi wa habari mjini Dodoma kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kilio hicho. Mkulo aliwaambia waandishi hao kwamba, ni kweli taasisi hizo zilikuwa zinapatiwa msamaha lakini imethibitika baadhi zinaitumia vibaya.

Misamaha ya kodi ambayo ilitolewa katika taasisi hizo na serikali kwa mujibu wa Mkulo ni bidhaa za kiroho, huduma za kidini, bidhaa za maendeleo ya kidini, afya na dawa kwa hospitali na kliniki ambazo zimesajiliwa.

Pamoja na kwamba, mapato ni muhimu ili kuiwezesha serikali kufanya shughuli zake za kimaendeleo kwa wananchi, serikali kwa namna moja au nyingine inatakiwa kuangalia umuhimu wa taasisi hizo kwa jamii pana.

Hata hivyo juzi serikali imetoa ufafanuzi kupitia Mamlaka ya Kodi nchini ikifafanua kuhusu misamaha ya kodi kw amashirika ya dini. Ufafanuzi huo unaelezwa na wachambuzi kuwa unalenga kuua mjadala kati ya serikali na dini.

Taarifa ya Mamlaka ya Kodi nchini iliyosainiwa na Kamishna Mkuu Harry Kitillya inaeleza kuwa vifaa ambavyo ni vya ibada pekee ndivyo ambavyo vitapata misamaha ya kodi.

Tena katika taarifa hiyo kuna ufafanuzi kuhusu misamaha katika vifaa vya afya na elimu, maeneo ambayo taasisi za dini zimejikita zaidi katika kusaidia kwenye shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment