KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

Tanzania yadaiwa kuwa na walemavu zaidi ya milioni 3


Na Happy Kulanga, Songea

INAKADIRIWA kuwa hapa nchini kuna walemavu zaidi ya milioni 3.7 miongoni mwa Watanzania wanaokadiriwa kuwa milioni 37 katika nchi nzima.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2002, inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya watu wote duniani wana ulemavu wa aina fulani.

Mkurugenzi wa shirika la walemavu linaloshughulikia haki za kisheria, maendeleo ya jamii na uchumi (DOLASED) lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam, Gidion Mandesi, aliyasema hayo mjini hapa wakati akizungumza na Mtanzania.

Kwa mujibu wa sensa ya watu hapa nchini ya mwaka 2002 watu wenye ulemavu ni 676,502, idadi ambayo alidai kuwa si sahihi, kwa kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa katika sensa hiyo kutokana na watendaji wake kutojua maana halisi ya ulemavu na mlemavu.

Kulingana na sensa hiyo, mtu mwenye ulemavu alichukuliwa kuwa ni yule ambaye ana upungufu katika moja ya viungo vyake vya mwilini, na hivyo kuhitaji usaidizi wa namna moja au nyingine katika utendaji wake wa kazi.

Alisema baada ya kubainika upungufu huo wa sensa hiyo pamoja na malalamiko kutoka kwa watu wenye ulemavu, serikali iliamua kuchukua takwimu za Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa serikali bado haijatoa kipaumbele kwa walemavu.

Alidai kuwa serikali inaonekana kutochukua lengo halisi la sensa kubaini uhitaji wa wananchi wake na kwa kiwango gani, ili iweze kutoa huduma muhimu za jamii, ikijumuisha mahitaji maalumu kwa watu wenye ulemavu.

Aliongeza kuwa kundi la walemavu hapa nchini ni kubwa na haliwezi kuachwa bila msaada na uangalizi kutoka serikalini na jamii kwa ujumla wake, kwa kupewa haki zote za msingi kulingana na mahitaji yao pamoja na kupewa nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi.

Mkurugenzi huyo wa DOLASED alitoa wito kwa jumuiya za watu wenye ulemavu na kwa serikali kuanza kufanya maandalizi mapema ya sensa ijayo ya taifa, ili kubaini idadi halisi ya watu wenye ulemavu nchini.

No comments:

Post a Comment