KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

Wasomi wachambua ubinafsi wa wabunge

Wasomi wachambua ubinafsi wa wabunge
:: Wakosoa namna wanavyochangia bajeti
:: Wasema wanatazama uchaguzi ujao pekee
:: Profesa Baregu aliita bunge la ‘marehemu’

Na Sarah Mossi

BAADHI ya wasomi wamekosoa aina ya uchangiaji mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2009/2010 unaofanywa na wabunge wakidai uchangiaji huo haulengi kuisaidia serikali katika kuinua uchumi wa kitaifa, badala yake unatazama kuwanufaisha wabunge ‘kisiasa’.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili juzi, wasomi hao walisema, mjadala wa bajeti unaofungwa leo mjini Dodoma haukulenga kutazama maslahi ya kunyanyua uchumi wan chi badala yake wabunge walitumia kila nafasi waliyopata kujinufaisha wao kisiasa kwa kuzungumza lugha tamu zinapendwa kusikika na wapiga kura.

Mmoja wa wasomi hao ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) Dk Richard Mushi aliliambia Rai kuwa; wabunge wengi hawakutazama jukumu lao la kutoa hoja za kitaifa badala yake wanawaza kuhusu uchaguzi mkuu unaofanyika mwakani.

Mhadhiri huyo alisema; “tungetegemea wabunge wasimame na kuzungumzia masuala kama fedha za Halmashauri ziongezwe, suala la barabara na sio kuzungumzia masuala yao ya majimbo pekee,” anazungumza na kuongeza:

"Kule bungeni kuna watu wachache wazuri sana, lakini sasa hivi wana presha kubwa ya kuchaguliwa mwakani na wanazikumbuka zile ahadi walizotoa katika uchaguzi mkuu uliopita."

Msomi mwingine aliyezungumza na Rai ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mwesiga Baregu ambaye alisema; sasa hivi wabunge hawawezi kuzungumzia masuala ya kitaifa kwa kuwa wanawaza zaidi majimbo yao.

Kufuatia hali hii, Profesa Baregu alifafanua kuwa, mahudhurio ya wabunge kwa sasa ni hafifu pia ukilinganisha na mabunge mengine yaliyopita na hii inatokana na hali ya wabunge kuwa na mguu mmoja ndani ya bunge na mwingine nje ya bunge.

“Hili si bunge la kujenga taifa. Ni la mkao wa uchaguzi wa mwakani, hata mahudhurio unayaona. Watatoka kwenda kwenye majimbo yao, hili ni bunge marehemu kwani nyoyo na fikra za wabunge zinatazama uchaguzi tu,” anasema Profesa Baregu na kuongeza:

"Sijui kama uwezo wao wa kuzungumzia masuala ya kitaifa kama ni mdogo ama vipi...Lakini ninachoweza kusema kwamba safari hii wanazungumza wengi na hata wale wanaolala hawatalala kwenye bunge hili. Akili zao zimeanza kuota kurudi ama kutorudi.

"Na hili angalau vyombo vya habari mmeliona mapema na mnapaswa kulipigia kelele, labda wanaweza kurudi," anasema Profesa Baregu.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mchumi Kitaaluma, aliliambia Rai kuwa wabunge katika bunge hili wameonyesha upeo mdogo wa mambo ya kitaifa.

"Lakini wengine wanaelewa wanachofanya, lakini wao ni wanasiasa wameweka mbele maendeleo ya maeneo yao. Wanataka wasikike kile wanachofanya sasa na tutarajie hilo na hapatakuwa na chochote cha kufanya na wao kama wanasiasa watataka wananchi wawasikie, hili ni jambo la kisiasa," anasema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alifafanua pia kuwa, wabunge wetu wameshindwa kujua yapi maeneo ya jumla na ya kipaumbele kwa sasa wanayopaswa kuzungumzia kwenye bajeti ya serikali. Eneo alilolitilia mkazo lilikuwa kuhusu Mkakati wa Serikali wa Kupunguza Umasikini (MKUKUTA).

"Huu ndio wakati mzuri wa kuzungumzia hoja za serikali pamoja na mipango yake ya uchumi, angalau wangeweza kuzungumzia mikakati ya jumla ya serikali kupunguza vifo vya mama na watoto, huduma za jamii, wangepaswa kwa sasa kuzungumzia yale mamabo ya kijumla ya kimaendeleo.

"Katika mambo yao ya majimbo wangeweza kujikita zaidi kwenye bajeti za kila wizara kwa mfano elimu, lakini hivi sasa wao wanaona huo ndio wakati wa kuzungumzia kwa vile watu wengi wanasikiliza. Kumbuka ule msemo wa mlio wa kwanza wa bunduki ndio wa kuukimbia, lakini kikubwa wanataka wasikike tu," anasema Profesa Lipumba.

Bajeti ya Serikali ilisomwa Alhamisi wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkullo na kuanza kujadiliwa na wabunge Jumatatu wiki hii. Mjadala wa bajeti hiyo unatarajiwa kufungwa leo jioni baada ya wabunge kupitisha vifungu vya matumizi kimoja baada ya kingine.

Katika bajeti ya mwaka 2009/2010, Serikali imepanga utekelezaji wa sera za matumizi kwa kulenga kuboresha kilimo na mifugo, kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida na umwagiliaji, pamoja na kuendeleza kuboresha huduma za elimu na afya.

Maeneo mingine ni kwenye miundombinu, viwanda, utalii, kuendeleza utafiti, kuendelea na utekelezaji wa kupeleka madaraka kwa wananchi, kugharamia uchaguzi wa serikali za mitaa, maandalizi ya uchaguzi mkuu 2010 na sensa ya watu na makazi 2012.

Mchanganuo wa bajeti katika sekta zilizotajwa uko hivi:

Elimu imetengewa Sh bilioni 1.743.9, ikilinganishwa na Sh bilioni 1.430.4 kwa mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 22. Kwa mujibu wa bajeti hiyo sekta hiyo inaendelea kuchukua sehemu kubwa ya bajeti kutokana na umuhimu wake.

Kilimo kimetengewa kiasi cha Sh. bilioni 666.9, ikilinganishwa na Sh. bilioni 513.0 za mwaka 2008/09, pamoja na fedha za marejesho za EPA. Sawa na ongezeko la asilimia 30.

Miundombinu imetengewa Sh bilioni 1.096.6, ikilinganishwa na Sh bilioni 973.3 mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 12.7. huku sekta ya Afya ikitengewa Sh bilioni 963.0, ikilinganishwa na Sh bilioni 910.8, mwaka 2008/09 sawa na ongezeko la asilimia 5.7.

Maji imetengewa Sh bilioni 347.3, ikilinganishwa na Sh bilioni 231.6 zilizotengwa mwaka 2008/09 swa na ongezeko la asilimia 50, huku sekta ya nishati na madini imetengewa Sh bilioni 285.5, ikilinganishwa na Sh bilioni 378.8 zilizotengwa mwaka 2008/09, sawa na upungufu wa asilimia 24.6. Hali hiyo imesababishwa na kumalizika mikataba ya kuzalisha umeme kwa makampuni ya kukodi ya Dowans, APR na Aggreko.

Kwa ujumla maeneo hayo muhimu kwa pamoja yametengewa Sh. biluioni 5,103.2, sawa na asilimia 64 ya bajeti yote ya mwaka 2009/2010.

No comments:

Post a Comment