KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

Manispaa kikwazo cha maendeleo

Uchumi

Na Waandishi Wetu

IKIWA wiki hii Ofisi ya Waziri Mkuu imesoma bajeti yake na kufuatiwa na hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), bado kunaonekana ugumu katika kufanikisha jukumu la kufikisha huduma za jamii kwa wananchi kutokana na kuwapo vizingiti kadhaa vinavyozisibu halmashauri na manispaa hapa nchini.

Ugumu uliopo ambao Rai imeubaini unasababishwa na utendaji butu katika halmashauri na manispa nchini, tatizo ambalo limekuwapo kwa kipindi sasa, huku kukiwa na nafasi finyu ya kupatikana tiba ya ya haraka ya tatizo hili.

Kwa mujibu wa ripoti na tafiti kadhaa ambazo Rai limefanikiwa kuzipitia hali inaonyesha kuwa, jitihada za serikali tangu awamu na awamu zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na halmashauri na manispaa nyingi kutokubaini majukumu yake vema.

Tena, ripoti zinaonyesha kuwa halmashauri na manispaa nyingi nchini zimekuwa zikifanya kazi kwa misingi ya kupokea amri kutoka Serikali Kuu, badala ya kusimamia majukumu yao moja kwa moja hasa yanayotazama maeneo ya huduma za jamii.

Ukiachia mbali miradi mikubwa inayosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu hasa ile inayohusu miundo mbinu, huduma za afya na elimu, miradi mingi inayobakia inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi ni ile inayosimamiwa na serikali za mitaa chini ya Halmashauri na Manispaa zake.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Taasisi ya Utafiti katika masuala ya Umasikini na Maendeleo (REPOA) iliyotolewa 2007, wananchi wengi katika matabaka yote ya jamii wanaonekana kukata tamaa kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu kadiri siku zinavyokwenda.

“Idadi kubwa ya wakulima, wafugaji na wavuvi wanaeleza kuwa hawapati msaada wowote kutoka serikalini,” inasema sehemu ya ripoti ya REPOA. Makundi haya yote yanategemea zaidi ufanisi katika Serikali za Mitaa na hivyo malalamiko yao yanaonyesha wazi kuwa, halmashauri na manispaa zina walakini katika kufanikisha jitihada za maendeleo.

Hoja za wananchi hawa zinaweza kuwa zinatokana na ukosefu wa wafanyakazi katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi. Na jambo hili linaweza kuthibitishwa na kauli ya Waziri wa Nchi (TAMISEMI), Celina Kombani ambapo katika hotuba yake bungeni wiki alisema: “Serikali imewapangia kazi watumishi wafuatao katika mwaka wa fedha 2008/09; Sekta ya Afya (2,380), Kilimo (856), Mifugo (168) na Uhasibu (200). Idadi hii ni ndogo ukilinganisha na upanukaji wa halmashauri, ongezeko la watu na utanukaji wa huduma.”

Ripoti ya REPOA inaonyesha mafanikio katika ujenzi wa shule za sekondari na inabainisha pia kuwapo ugumu wa kufanikisha mazingira ya utoaji wa elimu bora. Hali hii inatokana na kutokuwapo zana za ufundishiaji sambamba na upungufu wa walimu katika shule nyingi nchini.

“Asilimia 80 ya wanafunzi wa shule za msingi wa umri kati ya miaka saba na 14 hawapati huduma ya vitabu vya kujisomea, huku asilimia 15 tu ikipata huduma hiyo. Asilimia 60 ya walimu hawatokei madarasani kwenye vipindi vyao ama hawafiki kabisa shule,” ripoti ya REPOA inaeleza.

Katika huduma za afya, utafiti umeonyesha kwamba, asilimia 66 ya watu wanaugua malaria kila mwaka, asilimia 60 huugua kikohozi kitokanacho na mafua ama baridi, huku asilimia 32 wanaugua malaria. Magonjwa haya mengi yanawakuta wananchi maeneo ambako serikali za mitaa hupaswa kusimamia huduma za afya.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni nayo inabainisha kuwapo utata katika matumizi ya fedha hasa katika halmashauri na manispaa.

Ripoti hiyo licha ya kubainisha kuwepo kwa mabadiliko katika utunzaji wa kumbukumbu za fedha katika halmashauri na manispaa, pia inaffanua kuwa, mabadiliko haya yanatazama mbinu za utunzaji kumbukumbu za fedha tu, na sio uhalisia wa matumizi halali na yanayotazama vipaumbele.

Hali ya kutofahamu umuhimu wa vipaumbele ni tatizo linalokabili hata Bajeti Kuu ya Serikali. Kutokana na ugumu huu, ni jambo la wazi kuwa, huduma za jamii hasa maji, afya na elimu zinabaki kuwa nguvu kuwafikia wananchi hasa vijijini.

Maeneo ambayo yangetakiwa kuboresha maisha ya wananchi ili kufikia dhana ya maisha bora kwa kila mtu, hasa kilimo, ufugaji na uvuvi yanabaki yakipewa msukumo wa kisiasa zaidi ya uhalisia wake.

Kaulimbiu kama ‘Kilimo Kwanza’ iliyobuniwa hivi karibuni inaelezwa na baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na Chakula kuwa nayo ni mwendelezo wa kuingiza siasa katika masuala ya kitaalamu.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya Serikali za Mitaa ambao Rai imebahatika kuzungumza nao, ugumu katika hamlashauri na manispaa unabakia kitanzi kwa serikali ya rais Kikwete licha ya kuwapo nia ya kutaka kusawazisha mambo kabla ya uchaguzi ujao.

Ugumu huo unatokana na sababu moja kubwa, abayo ni kukosekana kwa utayari wa kukubali mabadiliko na pia utendaji unaotegemea picha ya uwajibikaji katika Serikali Kuu. Kama kunakuwa na upungufu katika uendeshaji wa Serikali Kuu, ni jambo la wazi kuwa Serikali za Mitaa zinabaki katika usingizi wa pono, hali ambayo inaathiri maeneo mengi ya Tanzania kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TAMISEMI; mfumo wa serikali za Mitaa Tanzania umewekwa katika misingi ya kutoa madaraka ya kisiasa, majukumu na rasilimali.

Serikali za Mitaa ni vyombo vinavyotekeleza majukurmu ya sekta mbalimbali (multi-sectoral corporate bodies) yaliyoainishwa katika sheria ya nchi.

Mamlaka za wilaya zipo 92 kwa sasa, mamlaka za miji midogo 3, mamlaka za miji 22 na halmashauri za vijiji 10,075 katika Tanzania Bara. Mamlaka hizi za Serikali za Mitaa zinaongozwa na wawakilishi waliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kupitia kwenye vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa.

No comments:

Post a Comment