KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 15, 2010

Wakati tatizo la umeme halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu nchini, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limetangaza mgawo wa umeme kwa mikoa sita.


Wakati tatizo la umeme halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu nchini, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limetangaza mgawo wa umeme kwa mikoa sita.

Mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa na Kati, itaathirika kwa kukosa umeme kwa muda wa siku saba kuanzia Mei 16 hadi Mei 23, mwaka huu.

Mgawo huo umekuja miezi minne tu tangu nchi ilipoingia gizani, baada ya kiwango cha uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa kupungua, baada mtambo wa Songas, Kihansi, Hale na Pangani kuharibika, mwezi Desemba mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa na Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana iliitaja mikoa itakayoathirika kuwa ni Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Mwanza na Mara.

Katika taarifa hiyo, Badra alisema mikoa hiyo itakosa umeme kutokana na kuzimwa kwa mitambo ili kuruhusu matengenezo ya kuboresha usambazaji wa umeme kutoka Gridi ya Taifa, upande wa Kaskazini Magharibi.

Alisema mgawo huo utakuwa wa awamu ambapo Mei 16 na 23, mwaka huu, umeme utakatwa kwa saa tisa mfululizo kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni ili kupisha matengenezo ya njia ya Dodoma/Singida ya msongo wa kilovoti 220.

“Pia tarehe 30 Mei na Juni 6, mwaka huu kituo cha kupooza na kusafirisha umeme cha Singida kitazimwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni. Mikoa itakayoathirika ni Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Mara,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Badra.

Alifafanua zaidi kuwa Mei 16 mwaka huu, Manispaa ya Tanga itakuwa gizani kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kwa kuwa Tanesco itazima mtambo wa Pangani unaohudumia njia ya kilovoti 132. Hata hivyo, tatizo la nishati ya umeme hapa nchini limekuwa kero kubwa kutokana na mgawo wa mara kwa mara kutokana na kuharibika kwa mitambo ya uzalishaji wa umeme na ukame kwenye mabwawa yanayotegemewa kuzalisha nishati hiyo.

Hali hiyo inaathiri sana shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali pamoja na matumizi ya nyumbani.

Oktoba mwaka jana, mgawo wa umeme uliokuwa wa saa 14 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:00 usiku, ulisababishwa pia na ukame kwenye baadhi ya mabwawa ya kuzalisha umeme pamoja na kuharibika kwa mitambo.

Kadhalika, Septemba mwaka jana, mikoa sita iliingia gizani kutokana na mgawo. Aidha, mwaka 2006, nchi ilikumbwa na mgawo wa kutisha baada ya maji kupungua kwenye mabwawa yanayozalisha nishati hiyo kutokana na ukame uliokuwa umeikumba nchi.

Mgawo huo uliilazimisha serikali kuingia mkataba tata na Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ya Marekani wa kuzalisha umeme wa megawati 100.

Hata hivyo, Richmond ilishindwa kuzalisha umeme huo na baadaye uchunguzi wa Kamati ya Bunge kubaini kuwa ilikuwa kampuni ya mfukoni licha ya mkataba wake wa miaka miwili kuigharimu nchi Sh. bilioni 200.

Licha ya mradi huo kugharimu fedha nyingi za walipa kodi, lakini pia ulivuruga hali ya kisiasa kutokana na kuwalazimisha mawaziri watatu kujiuzulu nyadhifa zao. Waliojiuzulu kwa shinikizo la Bunge kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Hadi sasa mbadala wa nishati ya umeme haujapatikana ingawa Tanesco iko katika mchakato wa kuagiza jenereta nne za kuzalisha umeme wa megawati 160 kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Mwanza.

No comments:

Post a Comment