KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, May 7, 2010

Urusi yawaachia maharamia wa Kisomali


Urusi imewaachilia huru maharamia wa Kisomali baada ya kutokea mapambano ya kuiokoa meli ya mafuta ya Urusi mapema wiki hii.

Waziri wa ulinzi wa Urusi amesema maharamaia hao wameachiliwa kutokana na upungufu uliopo wa sheria za kimataifa.


Marshal Shaposhnikov iliyosaidia kuokoa meli iliyotekwa na maharamia
Awali Urusi ilisema maharamia hao 10 wangepelekwa Moscow ambapo wangeshtakiwa kwa tuhuma za utekaji nyara.

Meli hiyo iitwayo Moscow University iliyokuwa imebeba mafuta ilitekwa nyara katika Ghuba ya Aden karibu na Yemen wakati ikielekea Uchina.

Urusi ni moja wapo wa nchi zilizoitia saini sheria ya Umoja wa Mataifa inayohusu maswala ya baharini ambayo inazipa nchi wanachama haki ya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka maharamia.

Hata hivyo baadhi ya nchi hazichukui hatua hiyo kwa sababu sheria hiyo haijaeleza maharamia hao wanapaswa kupelekwa wapi baada kutumikia vifungo jela.

Kuna zaidi ya washukiwa 100 wa uharamia wanaosubiri kesi zao zianze kusikilizwa na wengine tayari wamefunguliwa mashataka nchini Kenya. Lakini utaratibu huo unachukua muda mrefu sana na pia unagharimu pesa nyingi.

Kenya imesema inataka kurekebisha makubaliano kati yake na Umoja wa Ulaya, Marekani, Canada, Uchina na Denmark yanayohusu kesi za maharamia kwa sababu baadhi ya nchi hazijatimiza ahadi za misaada ya kifedha.

Baadhi ya washukiwa wa uharamia pia wamepelekwa Marekani, Ufaransa na Uholanzi ili kushtakiwa huko.

Ghuba ya Aden ni moja ya maeneo yenye shugli nyingi za safari za meli na Urusi, Marekani na Ulaya zimepeleka manuari za kivita kushika doria kutokana na kuongezeka matukio ya meli kushambuliwa na maharamia.

No comments:

Post a Comment