KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Friday, May 7, 2010

Mkutano wa uchumi wamalizika Tanzania


Mkutano wa Uchumi Duniani kanda ya Afrika uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam umemalizika, ambapo viongozi wa Afrika wamesema demokrasia inakua polepole katika nchi za bara hilo, licha ya kuibuka mfumo wa kuunda serikali za pamoja.

Hata hivyo, wamesema matunda ya demokrasia lazima yalete maendeleo ya kiuchumi na kusaidia kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya watu wa kawaida.

Mwandishi wetu wa Tanzania, Josephat Mwanzi aliyekuwepo kwenye mkutano huo amesema Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, alisema lazima demokrasia iendane na maendeleo kwa sababu watu hawawezi kula demokrasia ili waweze kuishi.

Rais Zuma ameonya, "Demokrasia siyo lelemama ambacho kinaweza kufanikishwa kwa njia ya uchaguzi pekee, bali inahusisha serikali imara zinazoongozwa na katiba."

Dr Salim Ahmed Salim, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika naye amesema, "Udhaifu mkubwa upo katika katiba, ambapo viongozi hubadili vipengele kadhaa ili waendelee kukaa madarakani."

Kwa kile kilichooneka kujitetea baada ya viongozi wa kisiasa kukosolewa zaidi, Raisi wa Msumbiji Amando Emilio Guebuza amesema wanapambana na umasikini kwa kujitahidi kuwa na utawala bora na kuzuia rushwa.

Washiriki kwenye mkutano huo wameonekana kusikitikitishwa na umasikini unaolikabili bara la Afrika, bara lenye raslimali nyingi muhimu ikiwa ni pamoja na raslimali watu ambao wanafikia bilioni moja, na asilimia 60 kati ya hao ni vijana.

Udhaifu mkubwa upo katika katiba, ambapo viongozi hubadili vipengele kadhaa ili waendelee kukaa madarakani
Dr Salim Ahmed Salim
Suala lingine lililojadiliwa ni hatua ya Afrika kuwa tegemezi licha ya kuwa na rasilimali nyingi.

Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga ameona bara la Afrika limepiga hatua katika demokrasia ukilinganisha na miaka 50 iliyopita huku akiwasihi viongozi kuachana na misaada ya magharibi.

Kauli yake hiyo imeungwa mkono na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na kutaka Afrika iache tabia ya kuomba.

Mbali na masuala ya uongozi bora na uchumi, kilimo nacho kimejadiliwa sana licha ya viongozi hao kutofautiana katika hoja mbalimbali.

Wakati Rais Kikwete akiona teknolojia na kuboresha mazao ndio vitu muhimu, waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi ameona bora kuwawezesha wakulima wadogo mwanzo na kuwapatia masoko.

Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dk. Kanayo Nwanze, amesema IFAD itawekeza dola milioni 165 nchini Tanzania zitakazotumika kusindika mazao na kutangaza bidhaa za Tanzania.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni Rais Armando Guebuza wa Msumbiji, Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Wengine ni Makamu wa Rais wa Burundi, Yve Sabinguvu, Rais wa Malawi, Rupia Banda pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha- Rose Migiro.

Katika hitimisho, wadau wa mataifa ya magharibi katika mkutano huo walisema Afrika inahitaji kujenga ushirikiano miongoni mwao na katika ngazi ya kimataifa ili kuondoa pingamizi zinazokabili nchi za Afrika.

No comments:

Post a Comment