KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

Taasisi za dini zakiri kufuja misamaha

:: Zataja wafujaji kuwa na uswahiba na viongozi
:: Yaelezwa iliwahi kuripotiwa kwa Tibaigana
:: Kamanda Kova akana kuzikuta taarifa hizo

Na Sarah Mossi

IKIWA ni wiki moja baada ya Serikali kukubali kurejesha misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa taasisi za dini, baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wamekiri kuwapo ufujaji wa misamaha hiyo.

Viongozi hao wameiambia Rai kuwa, kuna baadhi ya viongozi wa taasisi za dini wenye tabia ya kutumia vibaya misamaha hiyo. Inaelezwa kuwa, viongozi hao wamekuwa na tabia ya kuagiza bidhaa ambazo huishia kuuzwa katika ama maduka yao binafsi au yale ya wafanyabiashara ambao wana uhusiano nao.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, viongozi wa taasisi hizo zinazofuja misaada ni wale walio na uswahiba na viongozi wa serikali, hali inayoifanya serikali kubaki na kigugumizi cha kuwataja au kuwachukulia hatua.

Bidhaa zinazodaiwa kuingizwa na kisha kupata misamaha kabla ya kuingizwa sokoni ambazo Rai lina ushahidi wake ni mabusati, nondo, magari na mabati. Vifaa hivyo vyote huingizwa nchini kwa kisingizio cha matumizi ya taasisi za dini, lakini baada ya kuingizwa nchini, sehemu kubwa ya shehena hizo huuzwa kwa wafanyabiashara.

Baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na Rai wiki hii kwa masharti ya kuhifadhiwa majina yao, wameilaumu Serikali kwa kushikwa na kigugumizi na kutowachukulia hatua za kisheria watuhumiwa hao, licha ya kupewa taarifa za hujuma hizo.

Kiongozi mmoja wa msikiti maarufu jijini aliiambia gazeti hili kuwa, kiongozi mmoja wa msikiti wao (jina tunalo) alipata kukumbwa na kashfa ya kuingiza nondo kwa ajili ya ujenzi wa msikiti na magari mawili, lakini vifaa hivyo vilitumika kinyume cha matakwa yaliyokusudiwa.

Alisema baada ya uongozi wa juu wa msikiti huo kugundua hali hiyo, waliamua kumvua uongozi na kupeleka tuhuma na ushahidi wao kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, lakini hadi saa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya kiongozi huyo.

"Sisi kwetu tulimfukuza…na tukapeleka malalamiko yetu kwa Polisi, lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa na wanafanya hivi kwa vile wengine ni wapenzi wao," kilisema chanzo chetu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipotakiwa na Rai kuthibitisha kama ofisi yake ina kumbukumbu ya tuhuma za makosa yaliyowahi kupelekwa na viongozi wa taasisi za dini na kwamba imeshachukua hatua gani, alifafanua kuwa hana kumbukumbu hiyo.

"Sina tuhuma kama hizo, lakini sasa ni mwaka mmoja tangu Tibaigana aondoke na kwa kukusaidia tu ofisi yangu haipokei tuhuma kama hizo, kitengo cha makosa ya kughushi hupokea tuhuma hizi," alisema Kova na kukata simu.

Hata hivyo, Rai iliwasiliana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Abdallah Msika ambaye aliliambia gazeti hili kuwa, waliopeleka malalamiko yao kwa Tibaigana walitakiwa sasa kutoa taarifa zilizooonyesha namba ya jalada la malalamiko yao.

Alipoulizwa kuhusu suala la kuwapo wanaotumia vibaya misamaha ya kodi, alisema hataki kuliingilia kwa undani suala hilo.

Kiongozi mwingine wa ngazi za juu wa Dini ya Kiislamu naye alikiri kuwa zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutumia fursa ya misamaha ya kodi vibaya kwa kuingiza bidhaa ambazo hatimaye huuzwa madukani kwa wafanyabiashara.

Hata hivyo, kiongozi huyo alipotakiwa na Rai wiki hii kutaja taasisi hizo alikuwa mgumu na kusema asingependa kuchokoza mjadala huo kwani tayari vyombo vya sheria vimepewa taarifa za kiuchunguzi.

"Kwa hapa Dar es Salaam, baadhi ya taasisi si makini kabisa na siwezi kuzitaja kwa sasa labda serikali itachukua hatua," alisisitiza kiongozi huyo.

Katika Bajeti ya Serikali ya 2009/2010 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo Juni 11, mwaka huu, Serikali ilitangaza kuondoa misamaha maalumu ya kodi kwa asasi zisizo za kiserikali na mashirika ya dini.

Hatua hiyo ilihusisha taasisi zote za dini na serikali ikafafanua pia kuwa, vifaa vya kiroho na ibada vingeendelea kupata msamaha wa kodi.

Akisoma mapendekezo hayo ya serikali, Mkulo alisema misamaha ya kodi imekuwa ikiongezeka kwa kasi mwaka hadi mwaka na kufikia wastani wa asilimia 30 ya mapato ya kodi au asilimia 3.5 ya pato la taifa katika mwaka 2007/2008.

Alisema kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na viwango vya misamaha inayotolewa na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema katika nchi ya Kenya misamaha ya kodi inafikia asilimia moja ya pato la taifa, wakati Uganda ni asilimia 0.4 ya pato la taifa.

No comments:

Post a Comment