KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 24, 2010

INDIKETA UCHAGUZI 2010

:: CCM, CHADEMA, CUF vyabanana
:: Mikakati ya ndani na nje yaandaliwa
:: Ujana, usomi, ukabila vigezo vikuu
:: CHADEMA effect yaanza kutikisa
:: Wachovu watafutiwa warithi mapema

Na Waandishi Wetu

UKIWA umebakia mwaka mmoja Taifa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa nne wa vyama vingi unaofanyika mwakani, tayari mbio za kusaka nafasi mbalimbali zimeanza kubainika.

Katika toleo hili, Rai inaonyesha namna wanaotamani nafasi za ubunge katika Mkoa wa Dar es Salaam ambavyo wameanza kujiwekea mikakati ya ndani kwa ndani sambamba na ile ya nje, ikilenga kuhakikisha kuwa, wagombea binafsi sambamba na vyama vyao wanaibuka na ushindi.

Katika uchaguzi uliopita, Mkoa wa Dar es Salaam ulipata wabunge wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), licha ya kuwapo upinzani mkali uliotolewa na Chama cha Wananchi (CUF) kwa majimbo ya Temeke na Kigamboni na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimboni Ubungo.

Hata hivyo, upinzani mkali mkoani hapa ulikuwa ule wa kusaka wagombea kupitia CCM, ambapo Jimbo la Kigamboni lilishuhudia mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji akishinda kura za maoni na baadaye matokeo hayo kubatilishwa na mwisho wa safari kuibuka kwa Msomi Mwinchumu kama mgombea wa CCM, ambaye baadaye alifanikiwa na mwisho kushinda uchaguzi.

Hali katika jimbo hili kwa sasa inaonyesha upo uwezekano wa Mwinchumu kushindwa kurejea tena katika nafasi hiyo na tayari gazeti hili lina taarifa za ndani kutoka CUF, kinachojipanga kuhakikisha kinarejesha jimbo hilo ambalo awali kabla ya CCM lilikuwa likishikiliwa na mbunge wa chama hicho, Frank Magoba. Katika uchaguzi uliopita, CCM ilishinda jimbo hilo kwa asilimia 60 za kura huku CUF wakipata asilimia 35.

Hali hii ya ushindani bado inaonekana kuwa itatawala katika uchaguzi ujao na ni vyama hivi viwili vitakavyokuwa na ushindani mkali, iwapo tu CHADEMA hawatatumia mbinu wanazotumia CUF katika kuweka mgombea wao jimboni hapo.

Uchaguzi wa 2010 kwa mkoa huu wa Dar es Salaam, utajikita katika vigezo kadhaa na Rai imebaini kuwa, kwa baadhi ya majimbo suala la dini litabakia kutumika kama hoja ya kumbeba mgombea, huku pia katika majimbo mengine suala la uzawa, hasa kwa walio na asili ya Tarime na Kilimanjaro wakipata ahueni katika majimbo ya Ubungo na Ukonga.

Vigezo vya umri kwa maana ya vijana sambamba na elimu, pia vinaonyesha kuwa viashiria vya ushindi katika Jimbo la Ubungo kwa kuwa lina wapiga kura wengi ambao ni wasomi wa vyuo vikuu.

Hata hivyo, upo ushahidi wa kitafiti unaobainisha nguvu za baadhi ya vyama kwa sasa katika mkoa huu. Ni wazi kuwa vyama vya CCM, CUF na CHADEMA ndivyo vitakavyokuwa vikichuana vikali katika majimbo ya Dar es Salaam. Hali hiyo inatokana na CUF kuwa na ngome ya muda mrefu katika baadhi ya majimbo hasa Temeke na Kigamboni, huku CHADEMA ikionyesha kujenga heshima kwa kile kinachoitwa ‘CHADEMA effect’ sababu inayotokana na wabunge wa CHADEMA kuonekana kuwa mahiri katika kuzungumzia matatizo ya wananchi.

Jimbo la Ubungo ni wazi litakuwa na hamasa kubwa kutokana na kwamba, wapiga kura wengi hawaamini kama mgombea wa CHADEMA mwaka 2005 kijana John Mnyika (aliyepata asilimia 25) alishindwa na mbunge wa sasa Charles Keenja (aliyeshinda kwa asilimia 51). Hali ya Keenja jimboni humo, bado si ya kuonyesha nguvu za ushindi katika uchaguzi ujao na hali hii inatoa picha ya kuibuka washindani wapya kati ya CCM na CHADEMA.

Hadi sasa kwa upande wa CCM kuna hali ya kupigana kumbo kati ya makada kadhaa na hasa Nape Nnauye ambaye siku za hivi karibuni amekuwa na mikutano mingi katika jimbo hilo. Tayari kuna taarifa zinazobainisha kuwa kijana mwingine, Beno Malissa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) naye ana nia ya kuwania jimbo hilo.


Katika orodha ya wanaokusudia kuwania jimbo hilo licha ya kuwa hawajaweka hadharani nia yao, pia yumo Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga. Wanaomuunga mkono Mwangunga wanaamini kuwa ndiye aliye na uwezo wa kumzibia Keenja katika kura za uteuzi katika CCM.

Vigezo vinavyotumika katika kuvuta kura jimboni Ubungo ni pamoja na umri, ambapo mgombea kijana ana nafasi kubwa kutokana na jimbo hilo kuzungukwa na vyuo vikuu, kigezo cha lugha kinachotokana na wakazi wengi wa jimbo hilo kutokea mkoani Kilimanjaro, na kigezo cha elimu.

Vigezo hivi ndivyo vinavyotazamwa na baadhi ya wachunguzi na hata kuwafanya baadhi ya wagombea vijana kama Nape, Malissa na Mnyika kuonekana kuwa na nguvu katika uchaguzi ujao kama watapitishwa na vyama vyao.

Katika Jimbo la Ilala, bado kunaonekana kuwapo nguvu ya CCM na mbunge wa sasa Mussa Azan Zungu. Bado ana wakati mzuri kutokana na mgombea ambaye angekuwa mwiba kwake, Sofia Simba kukwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Nafasi hii inampa ubunge wa viti maalumu moja kwa moja.

Hata hivyo, jimbo hili bado linaonyesha kuwapo kukaliana kati ya vyama vitatu, ukianza na CCM, kisha CUF na kufuatia CHADEMA. Matokeo ya mwaka 2005 yaliipa CCM ushindi kwa asilimia 74, huku CUF ikifuata kwa kupata asilimia 19 na CHADEMA ilikuwa ya tatu na ikafanikiwa kupata asilimia nne.

Jimbo la Kawe, bado linaonekana kuwa na ugumu kutokana na mbunge wa CCM, Rita Mlaki ambaye kuna taarifa kuwa ana nia ya kurejea tena kuwa na kazi ngumu. Kazi hii inatokana na kukubalika kwake sambamba na chama chake hasa baada ya CHADEMA kuonekana kuwa chama kinachokuja kwa nguvu, huku tayari kukiwa na taarifa za wazi kuhusu Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (CHADEMA) kuonyesha nia ya kuwania ubunge kupitia jimbo hilo. Katika jimbo hili, nguvu inatarajiwa kuwa kati ya vyama hivi viwili yaani CCM na CHADEMA. Mlaki alipata kuwa naibu waziri, kabla ya mabadiliko yaliyomwacha nje, japokuwa kuachwa barazani hakumaanishi kushuka kwa hadhi ya mbunge husika.

Jimbo la Kinondoni linaloongozwa na mbunge Idd Azan wa CCM nalo bado linanyemelewa kwa udi na uvumba na CHADEMA. Chama hiki huenda kikamsimamisha mbunge wake wa viti maalumu, Suzan Lyimo katika uchaguzi ujao. Kwa upande wa CCM bado wanaozungumzwa kulitamani jimbo hili ni Abass Tarimba wanaoonekana kubaki kimya kwa sababu za kiufundi, huku pia Salum Londa, Meya wa Manispaa ya Kinondoni akitajwa kuwania jimbo hilo, huku kukiwa na taarifa pia kuwa analiwinda jimbo la Kibaha Mjini.

Jimbo la Temeke ambalo kwa vipindi kadhaa limekuwa na upinzani mkali kati ya CCM na CUF bado linaonekana kuendelea na hali hiyo. Hii inatokana na CUF kuwa na mtaji wa vijana wengi katika jimbo hilo na inaonekana wazi kuwa, uchaguzi ujao CCM watakuwa wakikabiliana zaidi na CUF ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.

Hata hivyo, mbunge wa sasa wa jimbo hili, Abbas Mtemvu anaonekana kuwa na hali tulivu, yaani kutoonekana kuharibu na pia kutokukubalika kwa kutisha ila kuna kila hali kuwa Tambwe Hiza ambaye alikuwa CUF na kuwania jimbo hilo mara kadhaa bila mafanikio na mara ya mwisho akipata asilimia 27.5 za kura, sasa anaweza kumkabili Mtemvu katika kura za maoni za CCM. Hiza kwa sasa ni Ofisa wa Kitengo cha Propaganda cha CCM.

Jimbo la Ukonga linaloongozwa na Makongoro Mahanga nalo linaonekana kuwa na hamasa hasa kutokana na CHADEMA kuonyesha nia ya kuwa na mgombea huko. Kigezo cha mgombea katika jimbo hili, ni pamoja na eneo la uzawa la mgombea, hasa wilayani Tarime mkoani Mara.

Kigezo hiki kinatokana na idadi kubwa ya wakazi katika jimbo hilo kuwa wenyeji wa Wilaya ya Tarime. Hadi sasa kuna taarifa kuwa, kada aliyehama CCM na kwenda CHADEMA, Mwita Mwikwabe Waitara anaandaliwa na chama chake kuwania nafasi hiyo. Uchuguzi wetu bado unaonyesha kuwa Mahanga ana nguvu katika CCM na pia kwa wananchi hasa kutokana na kuweka miundombinu katika maeneo mengi ya jimbo hilo. Alipata kuwa naibu waziri wa miundombinu, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa wadhifa huo huo.

No comments:

Post a Comment