KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 11, 2010

Saleh Kupaza: ‘mchawi’ Aliyepewa Mwana kulea Twanga Pepeta


WADAU wengi wa muziki wanajiuliza ni kwa nini mwaka 2008 bendi ya African Stars ‘Wana Twanga Pepeta ‘ ambayo ina kawaida ya kutoa na kuzindua albamu mpya kila mwaka, haikutoa wala kuzindua albamu katika mwaka huo.

Mengi yamekuwa yakizungumzwa huku wapenzi wengi wamekuwa wakidhani kuwa huenda Twanga Pepeta ilipoteza mwelekeo ama wanamuziki wake waliishiwa uwezo wa kutunga nyimbo mpya.

Ukweli hasa ni kwamba uongozi wa kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) chini ya Mkurugenzi wake mwanamama wa Shoka, Asha Baraka na wanamuziki wa bendi hiyo walikuwa na kiu kubwa ya kuzindua albamu katika mwaka huo wa 2008.

Lakini kiu hiyo ya uongozi wa ASET na wanamuziki wa Twanga Pepeta ilizimwa na mwanamuziki na mwimbaji mwenye uwezo wa kipekee, Saleh Kupaza maarufu kama ‘Mwana Tanga’.

Wakati wanamuziki hao wakiungana na Asha Baraka kutaka kutoa albamu, Kupaza ambaye sasa ndiye kiongozi wa bendi hiyo akishirikiana na Luiza Mbutu, alipinga wazo hilo la kutoa albamu katika mwaka huo.

Ni kwa nini mwanamuziki huyo ambaye kipaji chake kiliibuliwa na mwimbaji mkongwe na mwenye uwezo wa kipekee alipinga kuzindua albamu?. Kupaza anaeleza.

“Niliamua kupinga tusitoe albamu kutokana na ukweli kuwa mwaka 2008 bendi zilizokuwa zinatamba ni FM Academia na Akudo Impact. Ilikuwa unapokwenda kwenye maonyesho ya bendi hizo unakutana na watu nyomi (wamejaa) na huku kwetu lazima tuseme ukweli kulikuwa kunaonekana wazi kuwa kumetetereka,” anasema Kupaza.

Mawazo na akili za wapenzi wa muziki kwa wakati ule yalikuwa huko. Na mimi nachojua ili uweze kufanikiwa, kwanza lazima umkubali mwenzako anapofanya vizuri na wewe uiangalia kasoro yako. Sasa mimi sikuona kama ni jambo la busara kukurupuka kutoa tu albamu na kuzindua. Tulikuwa tunataka kujimaliza wenyewe,”

Kwa nini walikuwa wanajimaliza wenyewe , mwanamuziki huo anasema “Kwa kuwa akili za wapenzi wa muziki kwa kipindi kile zilikuwa katika bendi hizo mbili, nilihofia kuwa kama tungefanya uzinduzi, basi kulikuwa na uwezekano wa uzinduzi kuhudhuriwa na watu wachache".

“Hofu yangu ilikuwa zaidi kwa vyombo vya habari, kwani kama tungepigia viti, basi waandishi wangepiga picha na kutoa gazetini picha zikionyesha viti vikiwa vitupu na kutoa picha za zamani na za wakati huo na kicha cha habari kuuubwa, Ona Twanga ya zamani na ya sasa, kwisha kabisa” anasema Kupaza.

“Kwa hiyo uongozi walivyoitisha kikao na kutuambia tutunge nyimbo za kujaza albamu ili tufanye uzinduzi haraka, nilisimama na kuwaambia viongozi akiwemo Mkurugenzi kuwa Twanga hatuwezi kutoa albamu kwa mwaka huu. Kama mmezoea kupata pesa za uzinduzi kila mwaka, andikeni maumivu. Hakuna uzinduzi mwaka huu”

“Unajua uongozi ulishtuka, lakini walipokuja juu niliwafafanulia kwa nini nakataa. Niliwaeleza kama wanategemea pesa za uzinduzi, tutakapomaliza uzinduzi bendi itakuwa imekufa?. Na kama itakuwepo ina maana haitosimama?.

Niliwaambia kuwa lazima ifike mahali tuukubali ukweli kuwa FM na Akudo wako juu. Kwa hiyo badala ya kung’ang’ania kutoa albamu ili tuonekane na sisi tumo, ni vyema tukaa chini na kujipanga upya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Baadhi ya wanamuziki wenzangu walinielewa na kuniunga mkono, hali ambayo iliufanya hata uongozi wa ASET kulazimika kukubaliana na maamuzi hayo ingawa ilikuwa kwa shingo upande.

Kupaza anasema kuwa kwa kuwa uongozi ulikubali kwa shingo upande, hali ilikuwa mbaya kwa wanamuziki kwani kila walipokuwa wanaeleza shida zao uongozi haukuwa tayari kutoa pesa.

“Ilikuwa kila unapokwenda kuomba kitu unajibiwa pesa hakuna, hamjatoa albamu albamu mnadhani pesa tutatoa wapi. Lakini kwa kuwa tulikuwa tunajua tunachokifanya, hatukupaniki kwani tulijua itafika wakati uongozi utatuelewa na watatupongeza. Kwa hiyo tulielekeza nguvu zetu katika kufanya kazi,” anasema Kupaza.

Wahenga walisema penye nia pana njia na palipo na ukweli siku zote uongo hujitenga, mwaka 2009 Twanga ilianza kuachia nyimbo moja baada ya nyingine na hatimaye kuzindua albamu ya Mwana Dar es Salaam.

“Pale uongozi ndipo walipoelewa, kwani katika uzinduzi wetu pale Diamond Jubilee walijaa watu wengi sana. Naamini kama tungefanya hivyo mwaka 2008, watu wasingejaa vile” anasema Kupaza.

Kupaza anasema kuwa albamu ya Mwana Dar es Salaam ilianza kuwafanya wapenzi wa muziki ambao walianza kuchoshwa na mambo ya Akudo na FM hasa baada ya kugundua kuwa huko hakuna jipya, walianza kuigeuzia macho tena Twanga Pepeta.

Lakini wahenga walisema mgaagaa na upwa hali wali mkavu, na mchawi siku zote mpe mwana akulelee, baada ya Kupaza kuonekana adui mwaka 2008 kutokana na kushinikiza kutotoa albamu, uongozi wa Twanga umefurahishwa na shinikizo hilo ambalo limekuwa na faida kubwa na kuamua kumpa Kupaza uongozi wa bendi sambamba na mwanamama Luiza Mbutu.

No comments:

Post a Comment