KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

'Natamani kuwa mwimbaji mahiri' - Aaliyah

UNAPOZUNGUMZIA muziki wa dansi nchini hasa katika suala zima la taaluma ya unenguaji, utakuwa umefanya kosa kubwa kama kwenye mazungumzo yako hutomzungumzia Aaliyah Moses.

Mnenguaji huyu ambaye kwa sasa yuko na bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma', ni miongoni mwa wanenguaji mahiri na waliodumu katika fani hiyo kwa miaka mingi ambapo amekuwa mnenguaji kwa miaka 11 sasa.

Mwadada huyo alianza fani akiwa na umri mdogo mwaka 1998 katika kundi la Billbams lililokuwa linatumbuiza katika ukumbi wa Bilicanas jijini Dar es Salaam akiwa na vijana wenzake kama Hassan Nyemwela 'Super Nyamwela', Aisha Madinda na Omari Bokilo.

Lakini kwa sasa mwanadada huyo anataka kupiga hatua zaidi nayo si ingine bali kutoka kunengua huku akisindikizwa na sauti za waimbaji mbalimbali, na kuwa mmoja wa waimbaji mahiri na sauti yake ikiwa inawaongoza wanenguaji.

"Nimenengua kwa muda mrefu, nadhani sasa nahitaji kupiga hatua zaidi kutoka hapa nilipo. Nahitaji kuwa miongoni mwa waimbaji mahiri," anasema Aaliyah.

Jitihada za mwanadada huyo kutimiza malengo yake zimeanza kuonekana, kwani hivi sasa ameanza kushiriki kuimba nyimbo mbalimbali katika maonyesho ya bendi yake ya FM Academia.

"Nimeanza kuimba kidogo kidogo, naamini baada ya muda fulani nitakuwa muimbaji mahiri wa kike hapa nchini," anasema mwanadada huyo machachari awapo ndani ya jukwaa.

Ni sababu gani hasa zilizomfanya mwanadada huyo kutaka kuwa mwimbaji?.

Muziki uko kwenye damu yangu na muziki ndiyo maisha yangu. Nadhani hicho ndicho kinachonipa msukumo zaidi wa mimi kujifunza kuimba," anasema mnenguaji huyo.

Aaliyah anasema kuwa yeye anaamini kuwa atakuwa kwenye muziki katika kipindi cha maisha yake yote, lakini hawezi kuendelea kuwa katika muziki kwa kuwa mnenguaji.

"Umri unazidi kwenda. Naamini kabisa itafika wakati sitoweza tena kunengua. Itanilazimu kuachana na fani hiyo, lakini kama nikiwa mwimbaji nitaendelea kuwemo kwani uimbaji hauna umri," anasema.

Mwanadada huyo mwenye mtoto mmoja, alianza fani ya unenguaji mwaka 1998 kwenye kundi la Bilbams lililokuwa likifanya maonyesho yake katika ukumbi wa Bilicanas, akiwa na watoto wenzake kama Aisha Mohamed 'Aisha Madinda', Hassan Nyamwela 'Super Nyamwela' na Omari Bokilo.

Mwaka 2000 alijiunga na bendi ya The Millenium iliyokuwa ikiongozwa na Maroston Patcheko na mwaka 20001 alichukuliwa na mwanamuziki Kanda Bongoman kutoka Kongo na kufanya naye ziara ya kuzunguka bara la Afrika.

Mwaka 2002 alirejea nchini na kuchukuliwa na kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) na kuzitumikia kwa nyakati tofauti bendi zinazomilikiwa na kampuni hiyo, African Stars 'Twanga Pepeta' na African Revolution 'Tam Tam'.
Pia kwa nyakati tofauti amekuwa akienda Omani kufanya maonyesho.

Mwaka 2004 alijiunga na bendi ya Mchinga Sound iliyokuwa ikiongozwa na Ali Choki ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Extra Bongo.

No comments:

Post a Comment