KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, May 22, 2010

Blandina - Autosa Unesi Awe Msanii wa Maigizo

Suala hili halina budi kupewa uzito kwa sasa, kutokana na ukweli kuwa vijana wengi wanapelekwa kujifunza fani ambazo si zao huku vipaji vyao vikiachwa vinateketea.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa mwanadada Radhia Hassan Mtetemela. Mara baada ya kumaliza elimu yake ya Msingi katika shule ya Mwananyamala Kisiwani mwaka 2000, Radhia aliyezaliwa mwaka 1984 Morogoro vijijini, alipelekwa kusomea mafunzo ya Unesi.

Radhia anaweka bayana kuwa mafunzo hayo ya unesi aliyapata katika chuo cha Msimbazi Centre kilichopo Ilala jijini Da es Salaam mwaka 2006 na mafunzo yake ya vitendo aliyafanya katika hospitali ya Burhan iliyopo Posta jijini Dar es Salaam mwaka 2007.

Lakini pamoja na kupata mafunzo hayo ya unesi, bado Radhia hakuwa na shauku ya kufanya kazi hiyo kutokana na fani hiyo kutokuwa ndani ya damu yake. “Sikupenda kuwa nesi, kwa hiyo sikuendelea na kazi hiyo” anasema msanii huyo.

Baada ya kuachana na kazi hiyo, alikwenda kusomea mambo ya mapambo katika chuo cha ufundi stadi (VETA) kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Kama ilivyokuwa kwenye unesi, hata baada ya kuhitimu mafunzo hayo, hakuendelea na fani hiyo. “Bado kuna kitu kilikuwa kimenikaa ndani ya kichwa changu na niliona ndicho ninachostahili kufanya katika maisha yangu,” anasema Radhia.

Je ni kitu gani hicho?. Binti huyo mwenye umbo la kuvutia anaweka bayana kuwa sanaa hasa sanaa ya maigizo ndiyo iliyokuwa imemtawala kichwani mwake.

Tangu nilipokuwa mdogo nilipenda sanaa na nilijihisi kuwa nina kipaji cha kuigiza, kwa hiyo kila nililolifanya niliona kama napoteza tu wakati, lakini huku ndiko kwenyewe,” anasema msanii huyo.

Kutokana na hali hiyo, mwaka 2006 alianza kampeni zake za chinichini za kufanya sanaa kwa kujiunga na vikundi mbalimbali vya sanaa maeneo ya nyumbani kwao Mwananyamala.

“Kwa kuwa nilikuwa napenda sanaa lakini sijawahi kuifanya, ilinibidi nianze kwenye msingi, yaani kujifunza kwa kujiunga na vikundi mbalimbali kwa lengo la kupata uzoefu,” anasema msanii huyo.

Mwaka 2008 aliangukia katika mikono ya msanii mkongwe na mahiri hapa nchini, Mohamed Jengua ‘Mzee Jengua’ katika kundi lake la Kidedea lenye maskani yake Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alikaa na kundi hilo kwa muda wa mwaka mmoja lakini hakuweza kupata bahati ya kushiriki katika michezo yoyote ya kuigiza iliyotolewa na kundi hilo.

Kwa kuwa alikuwa na kiu ya kusaka mafanikio, mapema mwaka huu alijiengua katika kundi hilo na kujiunga na kundi la Amka Sanaa Group ambalo lilikuwa linaonyesha michezo yake katika kituo cha ITV.

Hata hivyo pamoja na kujiunga na kundi hilo, bado hakuweza kupewa nafasi kubwa ya kushiriki katika michezo iliyokuwa inatolewa na kundi hilo.

“Nikiwa na kundi hili tulitoa michezo zaidi ya miwili pale ITV, lakini sikuweza kupata nafasi, labda waliona kuwa sina uwezo wa kuigiza”

Lakini wahenga walisema mgaa gaa na upwa hali wali mkavu, na riziki ya mtu siku zote iko mikononi mwa mtu, kwani wakati Amka walikuwa hawamfikirii, milango aya mafanikio ikafunguka kwa upande mwingine.

“Nakumbuka siku moja nilikuwa niko mazoezini, kuna msanii mwenzetu anaitwa Omari alinieleza kuwa kuna rafiki yake anaitwa Seleman Mkangara anatafuta msanii wa kucheza katika filamu yake Blandina, hivyo kama sitojali anipeleke nikafanye majaribio.

“Kwa kweli nilishtuka niliposikia jina la Mkangara kwani huyu ni miongoni mwa waandaa filamu ambao ninawaheshimu. Kwa hiyo niliona nafasi yangu kwake ni ndogo, lakini Omari alinishawishi na kunisihi kuwa nikajaribu bahati yangu naweza kufanikiwa.

Msanii huyo anasema kuwa alipofika aliwekwa mbele ya kamera na kuanza kufanyiwa majaribio huku akiwa na hofu, lakini Mkangara alijaribu kumtoa hofu na kumfanya awe huru.

“Nilikuwa naogopa kutokana na watu wote walio mbele yangu ni wageni, lakini Mkangara alinitoa hufu na kunifanyia mambo ambayo yaliniondoa hofu na kufanya vyema.

Mara baada ya kumaliza alinieleza kuwa atanipigia simu kwani tulikuwa wengi tuliofanya majaribio kuwania nafasi hii. Baada ya siku mbili alinipigia simu na kunieleza kuwa nimepita, kwa kweli nilifurahi sana, kwani niliona sasa naanza kupata mwanga,”.

Msanii huyo anasema kuwa mara baada ya kusaini mkataba, alijikuta akiwa kwenye wakati mgumu hasa baada ya kupewa muongozo (script) ya filamu hiyo ya Blandina.

“Kwa kweli Blandina ni filamu ngumu kuicheza kwani inavitu vingi vinavyohitaji uhalisia na hisia za hali ya juu. Lakini nimefarijika kuona kuwa nimeicheza vizuri, nimejifunza mengi kupitia filamu hii,” anasema msanii huyo.

Radhia anasema kuwa anamshukuru sana Mkangara, kwani mbali ya kugundua kipaji chake, lakini ameweza kumjenga sana kisanii.

“Utakapoangalia filamu hii utaona nimecheza kwa kiwango cha hali ya juu, lakini ukweli nimetengenezwa na Mkangara na kwa kufanikiwa kuicheza filamu hii naona milango ya mafanikio kwangu sasa iko wazi".

No comments:

Post a Comment