KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

Said Fella, Kutoka Kwenye Upromota Hadi Kushika Maiki

Jina la Fella linajulikana kutokana na ushiriki wake katika muziki kwa zaidi ya miaka 10, akiwa kama meneja wa kundi la TMK Wanaume Family lenye maskani yake Temeke Dar es Salaam.

Fella alianza kuingia katika medani ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1990 akiwa kama meneja wa msanii Juma Kassim Kiroboto 'Juma Nature' na baadaye kundi la Wachuja Nafaka lililokuwa linawashirikisha Juma Nature, Rashid Ziada 'KR' na Doto Makala 'D-Chief'.

Lakini ujio wa kundi la TMK Wanaume Family lililoanzishwa Novemba 12 mwaka 2002, ndiyo uliomtambulisha na kumtangaza zaidi na hata kuwafanya wadau wengi wa muziki kumfahamu kuwa ni nani na ana nafasi gani katika muziki wa Tanzania.

Fella alibainisha kuwa walipoamua kuanzisha kundi la TMK Wanaume Family kwa kushirikiana na Juma Nature, KR, Karama Bakari 'Luteni Karama', D-Chief na wengine, hakuna aliyewapa nafasi kuwa ndoto yao ya kundi hilo kuwa miongoni mwa makundi makubwa ya muziki kama itafanikiwa.

Fella anasema kuwa sababu kubwa iliyofanya wadau wa muziki kutowapa nafasi, ni kutokana na maisha duni waliokuwa nayo wasanii wote waliokuwa wanaunda kundi hilo.

Fella anasema kuwa watu wengi walikuwa na mtazamo huo kwa kuwa hawakuwa wanajua lengo la kuanzishwa kwa kundi hilo.

"Unajua lengo la kuanzisha kundi hili, ni kuwasaidia vijana wetu kutoka katika maisha duni na kwenda kwenye maisha bora kwa kutumia vipaji vyao," anasema Fella.

Fella anasema binafsi alidhamiria kuwasaidia vijana hao, lakini hakuwa na uwezo wa kutoa pesa kwa kila mtu, ndipo aliamua kutumia kidogo alichonacho kuwakusanya pamoja vijana hao na kuviendeleza vipaji vyao.

"Ilikuwa ni kazi ngumu kwa kweli, lakini siku zote mvumilivu hula mbivu, baada ya kupata shida nyingi hatimaye tuliweza kusimama na TMK kuwa kundi linaloheshimika na kuogopeka katika medani ya muziki ndani na nje ya Tanzania," anasema Fella.

Wahenga walisema ngoma ikivuma sana, mwisho hupasuka, baada ya kupata mafanikio makubwa hatimaye kundi hilo lilisambaratika na kuanzishwa kwa TMK Wanaume Halisi linaloongozwa na Juma Nature.

Wasanii wengine walioondoka na Nature walikuwa ni Luteni Karama, D- Chief na Abdu Mzimu, ambao waliungana na Rich One, Inspekta Haroun ambapo wasanii hao waliamua kutunga wimbo wa Mshike Mshime Ndege Tunduni, wimbo ambao unadaiwa kuwa ni kijembe kwa Fella na kundi lake la TMK Family.

TMK Wanaume Family wakawajibu kwa wimbo wa 'Kazi Ipo' waliomshirikisha Aboubakar Katwila 'Q Chilla', wimbo ambao una maneno mazito ndani yake.

Wakati kundi hilo likiwa limerudisha heshima yake, mara wasanii watatu, Yesaya Ambukile 'YP', Y-Dash na Jebi nao walijitoa na kwenda kuanzisha TMK Unit, kundi ambalo limeshindwa kabisa kufurukuta katika medani ya muziki.

Kutokana na mafanikio waliyopata TMK Wanaume Halisi katika malumbano yao na Fella, akina YP nao waliamua kutumia silaha ya kumpaka matope Fella ili waweze kusimama, lakini hata hivyo hawakuweza kusimama wala kufurukuta.

Kama ulivyo ule msemo wa 'dawa ya moto ni moto, si maji, Fella ameamua kuingia ulingoni na kushika kipaza kuwajibu wasanii wote waliojitoa katika kundi hilo na kujaribu kumpaka matope, kupitia wimbo wake wa 2008/2009 unaopatikana katika albamu yake ya 'Mkubwa na Wanawe' iliyopo sokoni.

Mbali ya wimbo huo, katika albamu hiyo pia utakutana na nyimbo kama Ndugu Zetu, Nakshi, Kiboko Yao, Monalisa, Bila kampani, Naumwa Mapenzi, Tunapendana na Sabrina.

Ndani ya wimbo huo, Fella amemwaga mistari yenye maneno na ujumbe mzito, ujumbe ambao utakapousikiliza ndiyo utaamini kweli Fella hakukurupuka katika uamuzi wake wa kushika kipaza.

HEBU ONJA MASHAIRI YA WIMBO WAKE.

Nipe tano mwanangu, utacheka mwanangu
Iza kubonane, Iza uchwala manje
Under akija mpole, ukifanikiwa kumtoa tu
Ye kulonga tu
Anajisahau kweli kweli, siyo kwa dj
Mpaka kwa waandishi wa habari
Shida zote kasahau
Tanganyika ilianza halafu uhuru
Hivi hawakumbuki, au ujana tu
Mara utasikia, meneja wake hufai
Amekuja mchovu, anaondoka na gari
Aliyekuja na ndala, unachungulia mfuko
anaondoka na Timber
Aliyelala sebuleni kwao kwa wazazi
mimi nampangia chumba
Wahenga walisema tenda wema ujichenge
Ruge aliniambia hii kazi nzito
mimi nikamuambia brother labda kwako

UBETI WA PILI

Verse ya pili dekshia, hajakuja na msingi
leo anasema amedhulumiwa
Kuna maskani ya kweli, kuna jiwe la ujinga
utasiki, kundi zima unaua wewe
Wote mzigo mwanangu, jitoea
Wamekujua kwa ajili ya kundi pamoja na mimi
Akiwa kwangu sema mkubwa, kolingi nyingi
Baba na mama wamekufa,
kweli kushiba kuna matata
Jana ameshindia kahawa, leo anasema hajazoea shida
Kaambiwa punguza pombe, kabeba begi kajitoa
Maisha bora kwa watanzania ndiyo yanakuja
Maisha bora TMK hivi hamjayaonja?
... mashairi ya nyimbo yanaendelea.

No comments:

Post a Comment