KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Sunday, May 16, 2010

Mark Webber ashinda Monaco Grand Prix


Kama safari ni hatua, basi dereva Mark Webber kutoka Australia, amepiga hatua mbili kubwa kwa kupata ushindi wa pili mfululizo. Juma lililopita aliwika Hispania, kabla ya kutamba mwanzo mpaka mwisho katika mpambano wa Monaco Grand Prix ambao una sifa ya ajali nyingi na ugumu wa kumpita dereva aliye mbele - ingawa historia yake ni kubwa na ndoto ya madereva wote kushinda.
Jambo jingine la kujivunia kwa timu yake ya Red Bull ni kuwa madereva wake wawili, yaani Webber na Sebastian Vettel wameweza kuchukua nafasi mbili za kwanza; Robert Kubica kutoka Poland akikokota mashine ya Renault amekamata nafasi ya tatu.
Katika nafasi ya nne, ni Felipe Massa kutoka Brazil akisukuma mashine ya Ferrari; wakati mwingereza Lewis Hamilton wa Mercedes McLaren aliambulia nafasi ya tano, dereva mwenza Jensen Button, hakumaliza mpambano kutokana na gari yake kuchemsha.
Ushindani

Hata hivyo, sifa zitamwendea Fernando Alonso ambaye alianza mbio hizo akiwa dereva wa mwisho kati ya 24, lakini kwa kasi ya kipekee, na hesabu kali za muda wa kubadilisha magurudumu, alikwea kutoka mpaka ya saba hatua ambayo imemfanya aendelee kuwa na matumaini ya kutwaa taji mwisho wa msimu

Katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mashindano kumalizika, mshindi wa patashika hiyo, Mark Webber amesema kushinda Monaco si kazi rahisi na ni ndoto ya kila dereva.

Kwa ushindi huo, Webber sasa anaongoza katika msimamo wa ubingwa wa dunia, tayari amefikisha pointi 78, akiwa sawa Sebastian Vettel ingawa kashinda duru zaidi; na Fernando Alonso wa timu ya Ferrari ana pointi 73. Duru inayofuatia itawapambanisha madereva hao huko Uturuki tarehe 30 ya mwezi huu wa tano.

No comments:

Post a Comment