KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, May 12, 2010

Maharamia 'watoswa' baharini na kufa

Kundi la maharamia waliokamatwa na meli ya wanamaji wa Urusi wiki iliyopita na kuachiliwa huru wanadhaniwa kuwa wamekufa.
Maharamia tisa walikamatwa na meli ya kijeshi ya Urusi, siku moja baada ya maharamia hao kuteka meli ya mafuta ya Urusi katika Ghuba ya Aden.

Awali mamlaka za Urusi zilisema zimewashitaki maharamia hao, lakini baadaye iliarifiwa kuwa maharamia hao waliwekwa katika chombo kidogo cha baharini, mamia ya kilomita kutoka nchi kavu, na bila ya vifaa vyovyote.


Maharamia katika chombo

Taarifa zinasema mawasiliano kutoka katika chombo hicho yalipotea saa moja baada ya maharamia hao kuachiliwa huru.

Maharamia hao, waliotaka kuteka meli ya mafuta iliyokuwa ikielekea Uchina, walizidiwa nguvu na majeshi ya wanamaji wa Urusi.

Mashirika ya habari ya Urusi yanakariri taarifa za kijeshi zikisema wanajeshi wa Urusi waliwanyanganya silaha na dira maharamia hao kabla ya kuwaweka kwenye chombo kidogo cha baharini.


Taarifa hizo zinasema chombo hicho kilipotea na kilikuwa mbali na nchi kavu.

Mamlaka za Urusi zinasema zilichukua uamuzi wa kuwaachilia maharamia hao, baada ya kuona hakuna sababu kwa misingi ya sheria za kimataifa kuwapeleka Urusi na kuwashitaki mahakamani.

No comments:

Post a Comment