KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

Je Muziki wa Bongo Fleva Unakaribia Kupoteza Utamu Wake?

KUANZIA mwanzoni mwa miaka ya 2000, ubongo wa wa vijana wengi wa Tanzania ulikuwa umejaa muziki wa Bongo Fleva. Unapowaona wamekaa vijana zaidi ya mmoja, basi mazungumzo yao yalikuwa ni juu ya muziki huo.

Hata mavazi yao, matamshi yao yalikuwa ni ya kibongo fleva. Suruali kubwa inayoacha makalio wazi, fulana kubwa na hereni kifuani. Hiyo ndiyo ilikuwa staili ya kukuonyesha kuwa wewe ni mwana BongoFleva.

Uumini wa vijana katika muziki huo, uliwafanya wengi wao kuamua kuwa waimbaji wa Bongo Fleva, ambapo wenyewe wanaita kushuka mistari.

Katika mazingira hayo kila kukicha kukawa kunaibuka wasanii wapya. Hawa wanajiandaa kuingia studio, wale wanaingia studio, yule anatoka studio na wengine wanaanza kusikika kwenye vyombo vya habari, televisheni na redio pamoja na kupamba kurasa za magazeti.

Hakuna kilichofanyika zaidi ya muziki. Baadhi yao walidiriki hata kuacha masomo ili ada za shule walizopewa na wazazi wao wakalipie studio.

Hali haikuwa hivyo kwa vijana pekee, kwani hata watu wazima nao ubongo wao ulitekwa na Bongo Fleva, hasa kutokana na masikio yao kulazimishwa na watangazaji wa redio na televisheni kusikiliza muziki huo. Kila kona ni Bongo Fleva.

Lakini wakati muziki huo unachukua chati, mwanamuziki mkongwe na kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo 'Mjomba' alisema kuwa muziki huo ni sawa na Big G itafika kipindi utaanza kupoteza utamu.

Katika miaka ya hivi karibuni maneno hayo ya Gurumo kama yanaanza kutoa mwanga, kwani hali iliyouwa awali katika muziki huo inaanza kupotea.

Muziki huo umeanza kupoteza umaarufu wake kwenye vinywa vya vijana. Wengi waliokuwa na ndoto ya kuwa wasanii wa Bongo Fleva wameanza kurudi nyuma, huku wengi wao walioingia wanatoka.

Mavazi ya kibongofleva na swing (miondoko) ya kibongofleva yamepotea na wale ambao waliyatoa mawazo yao shuleni, sasa wameanza kuyarudisha.

Kana kwamba haitoshi leo hii ile kasi ya kusikika nyimbo mpya kila kukicha imepotea na hata zile zinazosikika ni chache zenye utamu. Nyingi zinakuwa ili mradi nyimbo.

Je kukosekana kwa matamasha na soko bovu la muziki nchini ndiyo sababu ya vijana kuanza kujitoa kwenye gemu la muziki huo?.

Joseph Haule 'Profesa Jay' na Ambwene Yesaya 'AY' wanakanusha hilo, na kusema kuwa woga na kutojiandaa kwa vijana ndiyo chanzo.

"Wengi wao walitaka kuingia kwenye gemu kwa kufuata pesa na umaarufu, lakini hawakuwa wamejiandaa kuwa katika safari hii watakutana na vikwazo vingi. Kubaki kwenye gemu kunahitaji ubishi na kujituma," alisema Profesa Jay.

"Kwa wale tuliojiandaa na tulioamua kufanya muziki kutokana na mapenzi bado tupo. Kwa mtu aliyejiandaa huwezi kuangalia soko la ndani pekee, lazima ujitafutie soko la nje," anasema AY.

Maneno ya wasanii hayo yana ukweli ndani yake, lakini pia yatumiwe kama dira kwa wanaotaka kuwa wana Bongo Fleva.

No comments:

Post a Comment