KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

Halima Ibrahimu - Mnenguaji Tegemeo wa Extra Bongo Aliyeanzia Kuimba Kanisani

Halima alipozaliwa mwaka 1985 kule Mbeya Vijijini, ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa mmoja wa waimbaji mahiri wa kwaya hapa nchini.

Ndoto yake hiyo ilitokana na kuvutiwa na mwimbaji kwaya mahiri mkoani Mbeya, Debora Mnisabira mwenye maskani yake Mbeya mjini.

Halima anaweka bayana kuwa alikuwa anavutiwa sana na uwezo mkubwa uliokuwa unaonyeshwa na mwanadada huyo katika uimbaji wa nyimbo za kumtukuza bwana.

"Nilikuwa napenda namna Debora alivyokuwa anaimba. Ana sauti nzuri na pia anaimba kwa hisia za hali ya juu. Kwa kweli na mimi nilijikuta nikishindwa kuvumilia na kuingia katika fani ya uimbaji kwaya," anasema Halima.

Alijiunga na kwaya ya kanisa la Asemblies of God na kuwa mmoja wa waimbaji wazuri wa kwaya ya kanisa. Kila mtu hakuaminia namna nilivyokuwa naimba.

Halima alikuwa anaimba kwaya huku akiwa anasoma katika shule ya msingi Mbeya Vijijini, kuanzia mwaka 1996 lakini ndoto yake ya kuwa mmoja wa waimba kwaya mahiri nchini, ilikatika mara baada ya kumaliza shule mwaka 2000.

"Mara baada ya kumaliza shule ya msingi nilioelewa. Kwa kuwa mume wangu alikuwa muisilamu, ilinibidi na mimi nibadili dini na kuwa muislamu, na ndipo nilipoitwa Halima," anasema mwanadada huyo.

"Baada ya kuolewa, nililazimika kuachana na mambo ya kuimba kwaya, kwani tayari nilikuwa katika dini nyingine ambayo hainiruhusu kufanya hivyo," anasema Halima.

Mwaka 2006 ndoa ya Halima ilivunjika rasmi na hapo ndipo alipoanza kuingia katika fani ya unenguaji huko maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam.

"Pamoja na kuimba kwaya, lakini pia nilikuwa napenda kucheza muziki. Kwa hiyo pale Manzese kulikuwa na kundi moja linalojihusisha na unenguaji nikaamua kujiunga nalo," anasema.

Lakini baadaye alijiunga na kundi la Bombeso lenye maskani yake CCM Mwinjuma, na huko ndiko alikokutana na mwimbaji Ally Choki, kipindi hicho akiwa na bendi ya TOT Respect.

"Sisi tulikuwa tunafanya mazoezi kwenye ukumbi wa CCM Mwinjuma, kwa hiyo Choki na baadhi ya wanamuziki wa TOT walikuwa wanakuja kutuangalia.

Siku moja Choki aliniambia, jitahidi kucheza ipo siku nitakuchukua katika bendi yangu. Kwa kweli mimi sikuyatilia maanani maneno yake, niliona kama utani tu," anasema Halima.

"Lakini siku moja alitimiza ahadi yake na kunifuata nijiunge na Extra Bongo, niliona kama ndoto. Sikuwa nafikiria hata siku moja kuwa nitakuja kuwa mnenguaji wa bendi kubwa kama hii ya Extra Bongo," anasema Halima.

Msanii huyo anasema kuwa mara baada ya Choki kumfuata, alimpigia simu mama yake na kumueleza, na mama yake alimpa baraka zote.

"Mama anampenda sana Choki, huwa anazisikiliza sana nyimbo zake. Nilipomueleza alifurahi na kunieleza kuwa niwe makini katika kazi," anasema Halima.

Msanii huyo anasema kuwa kujiunga kwake Extra Bongo kumempa mwanga wa mafanikio, hasa baada ya kujikuta akiwa pamoja na mwimbaji Khadij Mnoga 'Kimobitel' ambaye anadai kuwa alikuwa anamzimia miaka mingi.

"Kwa waimbaji wa dansi, nampenda sana Mnoga, anaimba vizuri, sauti yake ina mvuto na hana papara. Naamini nami siku moja nitatoka katika unenguaji na kuwa mmoja wa waimbaji mahiri wa bendi hii kama yeye," anasema Halima.

Mnenguaji huyo amewataka wadau wa muziki nchini kuipokea kwa mikono miwili Extra Bongo, kutokana na kile alichodai kuwa wanakuja na vitu tofauti.

"Tumejiandaa vyema na napenda kuwaeleza wapenzi kuwa tunakuja na watupokee kwa mikono miwili.Tumejiandaa vyema, hasa mimi binafsi napenda kuwaeleza kuwa nakuja kuwapa mambo makubwa," anasema msanii huyo.

No comments:

Post a Comment