KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

Safari Ndefu ya Muafrika wa Kwanza Kunyakua Medali ya Dhahabu Kwenye Olimpiki

INGAWA michuano ya Olimpiki ilianza rasmi karne ya nane kabla ya kuzaliwa Kristo hadi kuanza kujulikana rasmi karne ya tano baada ya Kristo, Waafrika walikuwa wakiisikia kwenye bomba tu hadi mwaka 1960 alipoibuka kijana wa kiafrika.

Kijana huyo si mwingine bali ni Abebe Bikila ambaye alichaguliwa kwenye timu ya Ethiopia iliyoshiriki Olimpiki dakika chache kabla ndege iliyobeba kikosi cha timu hiyo kwenda Rome haijaondoka, alichukua nafasi ya Wami Biratu, ambaye aliumia kifundo cha mguu katika mechi ya mchezo wa soka.

Meja Onni Niskanen aliwachukua Bikila na Mamo Wolde kwa ajili ya kukimbia mbio ndefu, zijulikanazo kama Marathon.

Wadhamini waliotoa viatu kwa wanamichezo wa Olimpiki ya mwaka huo, walikuwa wamebakiza jozi chache hivyo Bikila alilazimika kwenda kuangalia kama atapata vya kumtosha na mwishowe akaambulia pea moja tu ambayo nayo pia haikuweza kumtosha vizuri.

Kwa sababu hiyo, hakutumia viatu hivyo kwenye michuano hiyo na saa chache kabla ya mbio hizo, iliamualiwa Abebe akimbie pekupeku.

Bikila alionywa na Niskanen kuhusu wapinzani wake ambao mmojawao alikuwa ni Rhadi Ben Abdesselam wa Morocco, ambaye alitarajiwa kuvaa jezi namba 26.

Kutokana na sababu ambazo hazikufahamika, Rhadi hakwenda kuchukua jezi aliyotakiwa na alisisitiza kuvaa jezi yake ya kawaida namba 185.

Baadaye kabisa mchana, zilipokaribia kuanza katika eneo la Arch of Constantine, nje ya Colosseum, mwanariadha wa Australia, Ron Clarke alizungumzia juu ya Bikila kukimbia pekupeku.

Wakati wa mbio, Bikila aliwapita wakimbiaji kadhaa akitafuta mtu aliyevaa namba 26 na baada ya kilomita kama 20, Bikila alijikuta anachuana na mtu aliyevaa namba 185 wakiwa wanaachana kwa umbali mdogo mno.

Lakini Bikila aliendelea kukimbia kumsaka huyo aliyevaa namba 26, ambaye alikuwa hamfahamu hata kwa sura hivyo hakujua kama ni mtu anayekimbia kulia kwake.

Waliendelea kukimbia bega kwa bega hadi mita 500 za mwisho wakati Abebe alipoongeza kasi na kumaliza wakati mpinzani wake, Rhadi alimaliza sekunde 26 baadaye.

Bikila alishinda kwa kutumia muda wa saa 2: dakika 15, sekunde 16.2 na kuweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa Medali ya Dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki.

Baada ya mbio hizo, wakati Bikila alipoulizwa kwa nini alikimbia bila viatu, alijibu: “Nilitaka dunia ijue kwamba nchi yangu Ethiopia hushinda kwa kujituma na ushujaa."

Niskanen baadaye alipata taarifa kwamba, ikiwa Rhadi asingekimbia kwenye mbio za mita 10,000 siku chache kabla ya mashindano hayo, mbio hizo zingefutwa.

Bikila alirejea Ethiopia kama shujaa na Wahabeshi walitamba kwa kusema; “Iliwachukua mamilioni ya Wataliano kuvamia Ethiopia, lakini askari mmoja wa Ethiopia aliiteka Rome,”.

Mfalme wa nchi hiyo, Haile Selassie alimpandisha cheo hadi kuwa Koplo sambamba na kumzawadia Medali ya nyota wa Ethiopia.

Muda mfupi baada ya michuano ya Olimpiki, Jeneral Mengistu Neway alipanga kufanya mapinduzi na Bikila, ambaye alikuwa haelewei lolote kuhusu siasa na pamoja na kushinikizwa kushiriki, mwanariadha huyo alikataa kuuwa walengwa na wakati jaribio la mapinduzi hayo liliposhindikana, wote waliohusika walipewa adhabu ya kifo.

Lakini Bikila alisamehewa na Mfalme wa nchi hiyo, baada ya watu wengi kujitokeza kumuombea msamaha.

Mwaka 1961 Bikila alikimbia Marathon nchini Ugiriki, Japan na katika Jiji la Kosice nchini Czechoslovakia, ambako kote alishinda.

Kati ya Oktoba mwaka 1961 na Aprili 1963 hakushiriki mashindano yoyote ya kimataifa kabla ya kujitosa kwenye Boston Marathon mwaka 1963 na kushika nafasi ya tano, hicho kikiwa kipindi kipekee alichoshiriki mbio hizo ndefu bila kushinda.

Alirejea Ethiopia na hakushiriki mashindano yoyote hadi ilipowadia michuano ya Addis Ababa mwaka 1964, ambako alishiriki na kushinda kwa kutumia muda wa saa 2: dakika 23, sekunde 14.

Siku 40 kabla ya michezo ya Olimpiki mwaka 1964 mjini Tokyo, japan, akiwa kwenye maandalizi, mjini Addis, Abebe Bikila alianza kusikia maumivu.

Kutokana na kutojali juu ya maumivu hayo na kuendelea na mazoezi, alizimia na kukimbizwa hospitali ambako alikutwa na ugonjwa wa kidole tumbo na baada ya kutibiwa alijisikia vizuri. Alianza taratibu kukimbia kimbia kwenye eneo la hospitali.

Katika michuano ya Olimpiki 1964, Abebe alikwenda Tokyo na ingawa kwa hali yake hakutarajiwa kukimbia, lakini alijitosa kwenye kinyang’anyiro safari hiyo akikimbilia viatu vya Asics.

Alitumia mbinu ile ile ya mwaka 1960 kukaa na vinara hadi kilomita 20 kuelekea mwisho aliongeza kasi. Baada ya kilomita 15 alijikuta yupo na Ron Clarke wa Australia na Jim Hogan wa Ireland. Muda mfupi kaba ya kubakisha kilomita 20, alimpangua kwanza Hogan, kisha Kokichi Tsuburaya wa Japan aliyekuwa nafasi ya tatu kabla ya kuingia kwenye Uwanja wa Olimpiki akiwa peke yake na kupokewa kwa shangwe na umati wa watu 70,000.

No comments:

Post a Comment