KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, February 9, 2010

Kisanduku cha ndege ya Ethiopia chapatikana




Vikosi vya uokozi nchini Lebanon vimefanikiwa kupata kisanduku cheusi kilichokuwa kikitumika kutunza kumbukumbu katika ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka katika mwambao wa Mediterrania hivi karibuni, maafisa wanasema.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737 ilianguka mnamo tarehe 25 Januari, muda mfupi baada ya kuruka kutoka uawanja wa ndege wa Beiruti wakati hali mbaya ya hali ya hewa, na kuwaua abiria wote 90 waliokuwemo katika ndege hiyo.

Afisa mmmoja wa jeshi amesema kisanduku hicho kimepelekwa katika kituo cha jeshi la wanamaji mjini Beiruti ili kukabidhiwa kwa wachunguzi wa ajali.

Kazi ya uokozi bado inaendelea kutafuta miili na kisanduku cha pili cha kumbukumbu katika eneo la ajali.

Waziri wa Usafirishaji nchini Lebanon Ghazi Aridi, alitangaza siku ya Jumamosi kuwa waokozi wamefanikiwa kugundua eneo viliko visanduku hivyo katika kina cha urefu wa mita 45 katika mwambao wa kijiji cha Naameh, karibu na kusini mwa uwanja wa ndege wa Beiruti.

Tokea wakati huo, waokozi wameweza pia kupata mabawa ya nyuma ya ndege hiyo na kazi imekuwa ikiendelea kuyaleta katika nchi kavu, afisa wa jeshi amesema.

Sababu ya ajali hiyo bado haijajulikana, hata hivyo maafisa wa Lebanon wamesema ndege hiyo haikufuata mwelekeo kama ilivyoelekezwa na kituo cha kuongoza ndege cha Beiruti wakati ikiruka.

Kisanduku hicho huenda kikaleta mwanga kujua ni kwanini rubani wa ndege hiyo alishindwa kufuata maelekezo aliyopewa wakati wa kurusha ndege, ingawaje alitambua maelekezo hayo.

Miili 15 imeopolewa kutoka katika ajali hiyo, lakini kwa mara kadhaa hali mbaya ya hewa imekuwa ikikwamisha zoezi la uokoaji katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

No comments:

Post a Comment