KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, October 5, 2009

Uchovu wamlemea Rais Kikwete, Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe. jitihada yako juu ya nchi yako anaishuhudia na ni alama juu ya kila njia ya mafanikio .


Rais wa Tanzania Dr. Jakaya Kikwete , siku ya Jumapili alilazimika kukatiza hotuba yake ghafla akionekana mchovu, na kuomba kuhutubia akiwa amekaa, jambo ambalo hata hivyo alilikatiza na baadaye kuondolewa kwenye jukwaa katika uwanja CCM kirumba mjini Mwanza na kwenda chumba maalum kwa ajili ya mapumziko mafupi.


Hali hiyo imetokea wakati Rais Kikwete akihutubia maelfu ya waumini wa kanisa la Africa Inland Church Tanzania katika madhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kanisa hilo nchini.

Rais Kikwete alikatisha hotuba yake baada ya kutojisikia vizuri huku sauti yake ikisikika kudhoofu kama mtu ambaye amepatwa na matatizo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema Rais Kikwete alilazimika kupumzika kutokana na kuzidiwa na uchovu kufuatia shughuli nyingi mfululizo katika siku za karibuni. Hata hivyo baada ya mapumziko ya muda aliendelea kushiriki katika shughuli hizo hadi mwisho.

“Nguvu imerudi…napenda sasa kuchukua nafasi hii kuzindua rasmi uchangiaji wa shughuli za Kanisa lenu na mimi naanza na mchango wa sh. 1,000,000,” Rais Kikwete aliwaambia maelfu ya waumini wa AICT huku wakimshangilia kwa nguvu mara aliporejea jukwaani.



Rais Kikwete alianza kusikia uchovu wakati akisoma hotuba yake mbele ya maelfu ya waumini wa Kanisa hilo. Rais huyo amekuwa na shughuli nyingi na hajapumzika katika miezi kadhaa iliyopita kutokana na kazi nyingi na ratiba ya shughuli za mfululizo.

Aidha ndani ya siku 15 zilizopita, Rais Kikwete amekuwa New York nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, na kwa siku mbili zilizopita alikuwa mjini Arusha kabla ya kwenda mjini Mwanza na leo kuhudhuria maadhimisho hayo ya Kanisa la AICT.


“Kwa kweli mshituko huu wa leo ni matokeo ya ubishi wangu. Nilishauriwa na wasaidizi wangu nipumzike baada ya kurejea nyumbani kutoka Marekani. Niliambiwa nisiende Arusha ama kuja hapa. Lakini nikakataa. Siku nyingine nitawasiliza zaidi.”

Rais Kikwete aliondoka kwenda Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) Septemba 20 na tokea hapo hajapata kupumzika. Alirejea nchini kutoka Marekani saa saba usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya kuwa amesafiri kwa zaidi ya saa 19 na asubuhi ya Ijumaa akasafiri kwenda Arusha kufungua Mkutano wa 55 wa Wabunge wa Jumuia ya Madola.



Rais alikuwa amepangiwa kurejea Dar es Salaam baada ya shughuli ya Arusha, lakini akalazimika kwenda Mwanza kwa shughuli ya Kanisa la AICT kwa sababu Waziri Mkuu aliyekuwa amepangiwa na Rais kushiriki shughuli hiyo alipewa kazi nyingine na Rais.

Hii ni mara ya pili rais Kikwete kupatwa na hali kama hiyo. Mara ya kwanza hali kama hiyo ilijitokeza wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka 2005 katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam. Wakati huo Rais Kikwete alikuwa akihutubia mikutano ya kampeni huku akiwa amefunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa jijini Mwanza hili ni tukio la pili kumtokea Rais Kikwete akiwa katika uwanja wa CCM Kirumba baada ya mtu mmoja kumvamia alipokuwa katika mkutano wa kampeni 2005 wakati akiomba kura kwa wakazi wa Mwanza. Mtu huyo alishtakiwa na kufungwa baada ya kukutwa na hatia ya kumshambulia mgombea urais wakati wa kampeni.

Wakati huo huo, Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) imetangaza kuwa itaangalia upya ratiba ya Rais wa Tanzania kwa lengo la kumpungumzia mlundikano wa shughuli.

Ofisi hiyo ndiyo husimamia kupanga ratiba za Rais. Baada ya tukio la hilo imetangaza rasmi kuwa inaangalia upya ratiba nzima ya matukio yajayo ili kuyapunguza na kumpa muda zaidi wa kupumzika.

No comments:

Post a Comment