KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, October 5, 2009

Annan ziarani Kenya kutathmini mabadiliko


Aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan anakwenda tena nchini Kenya kutathmini hatua zilizopigwa katika kufanya mabadiliko muhimu yaliyoahidiwa baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi mapema mwaka uliopita.
Bwana Annan alikuwa mpatanishi kati ya pande mbili hasimu na aliwezesha kuundwa kwa serikali ya kugawana madaraka,hali iliyotuliza taifa la Kenya kufwatia machafuko ya kikabila yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja.

Atakutana na wanasiasa,wanadiplomasia, mashirika ya kiraia na wafanyabiashara.

Ni wazi kuwa bwana Annan hatoridhishwa na kukosekana kwa maendeleo katika shughuli nzima ya mabadiliko.

Wakati mkuu huyo wa zamani wa umoja wa mataifa aliposaidia kuleta amani februari mwaka jana, wanasiasa kutoka pande zote mbili walikubaliana kuchukua hatua ambazo zitahakikisha kuwa taifa linabaki katika njia ya amani zaidi.

Waliahidi kufanya mabadiliko katika idara ya mahakama,jeshi la polisi na katika mfumo wa uchaguzi.

Takriban watu laki tatu walikimbia makazi yao kwa sababu ya machafuko baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Pia waliahidi kuunda katiba mpya na kutatua suala la umiliki wa ardhi,linaloonekana kuwa chanzo cha uhasama wa kikabila nchini Kenya.

Ahadi ya kuona kuwa waliochochea machafuko hayo wamefikishwa mahakamani pia ilitolewa.

Lakini hatua imekuwa ndogo hadi mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu (ICC) ikatangaza wiki iliyopita kwamba itawashtaki baadhi ya washukiwa wakuu wa machafuko hayo.Inadhaniwa kuwa hawa ni wanasiasa na wafanyabiashara mashuhuri.

Kwa hivyo Kofi Annan ataonyesha kutoridhishwa kwake na wanasiasa.

Wasiwasi wa kisiasa

Wakenya wengi watafanya hivyo.Kuna dhana miongoni mwa sehemu kubwa ya wakenya kwamba punde tu wanasiasa walipopata nyadhifa zao katika serikali ya muungano yenye gharama kubwa,wengi wao walianza kushughulika na mustakabala wao kuliko mustakabala wa taifa.

Badala ya kutatua matatizo yalosababisha ghasia katika uchaguzi mkuu uliyopita,baadhi yao wamekuwa waking'ang'ania nyadhifa kabla ya uchaguzi mkuu ujao mwaka 2012 - hata wengine kutangaza nia yao ya kuania urais.

Ili kuweka shinikizo,Kofi Annan itabidi atumie nafasi yake kwa uangalifu.

Alisaidia kupata ufumbuzi lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipinga namna anavyoendelea kulaumu hatua ndogo za marekebisho wakimshutumu kwa kuingilia masuala ya ndani ya Kenya.

Marekani na nchi za bara ulaya zinapata shutuma kama hizo wakati wanapotilia mkazo suala la marekebisho,wakitoa vitisho vya kuwanyima vibali vya kusafiri katika nchi zao wale walio vikwazo kwa marekebisho.

Lakini katika mitaa ya Kenya kuna fikra kwamba wanasiasa wanahitaji shinikizo kutoka nje hasa kwa sababu kuwepo kwa serikali ya muungano,hakuna upinzani wa kweli.

Kimsingi kuandamwa huku kwa wanasiasa kumewaridhisha wengi.

No comments:

Post a Comment