KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, September 9, 2009

Zimbabwe kuondolewa vikwazo


Viongozi kutoka kanda ya Kuisni mwa Afrika wamemaliza mkutano wao uliofanyika katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo
wameitaka jamii ya kimataifa iondoe vikwazo vyote dhidi ya Zimbabwe.
Viongozi hao kutoka nchi muungano wa SADC wamesema Zimbabwe imepiga hatua katika kuunda serikali ya muungano.

Wadadisi wamesema taarifa ya SADC ni ushindi kwa rais Robert Mugabe ambaye amekuwa akipinga kuwepo kwa vikwazo hivyo.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamesema kuondolewa kwa vikwazo hivyo kutasaidia wananchi ambao wameendelea kutaabika kutokana na hali ya sasa.

Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulitoa taarifa ikisema, ''Hatua muafaka zimepigwa katika utekelezwaji wa mktaba wa kisiasa ulioafikiwa kimataifa nchini Zimbabwe''

Taarifa hiyo iliendelea,'' Ipo haja basi kwa jamii ya kimataifa kuviondoa vikwazo vyote dhidi ya Zimbabwe''.

Waziri mkuu wa Zimbabwe hajazungumzia lolote kuhusu taarifa hiyo.

Msemaji wa rais Mugabe Geroge Charamba amepongeza taarifa hiyo na kusema '' Vikwazo vyote dhidi ya Zimbabwe siyo haki na ni haramu''

Msimamo wa SADC umeonekana kupuuza kauli ya waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai aliyependekeza kuwepo kikao maalum kutathmini hatua zilizopigwa tangu kuundwa kwa serikali ya muungano.

Wito huo ulikataliwa na viongozi wa SADC.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye amekuwa mkosoaji wa bwana Mugabe katika siku za awali alitarajiwa kuunga mkono Tsvangirai alisema hakuna masharti yanayostahili kuwekwa katika kuviondoa vikwazo vya sasa.

''Tunachosema ni kwamba kwa kuviondoa vikwazo kutasaidia mpango wa utekelezwaji wa makubaliano yaliyoafikiwa na pande zote nchini Zimbabwe'', Alisema Zuma.

Mdadisi wa kisiasa Geoff Hill amesema bwana Zuma aliitikia shinikizo kutoka kwa wanasiasa wenzake wa SADC.

Ameambia BBC kuwa viongozi wengi wa SADC wanahofu huenda msimamo wowote dhidi ya Zimbabwe ukatumiwa dhidi yao siku za usoni.

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema ni mapema sana kuviondoa vikwazo hivyo likisema madaraka yangali mikononi mwa wale wanaowadhulumu watu.

'' Mugabe amefanikiwa kuwashawishi viongozi wa SADC kutaka jamii ya kiamataifa iondowe vikwazo bila kuzingatia hali ya haki za kibianadamu nchini Zimbabwe'' amesema afisa wa shirika hilo Geogette Gagnon.

No comments:

Post a Comment