KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, September 25, 2009

Nchi za G20 kuratibu uchumi wa dunia


Kundi la nchi G20 zilizoendelea zaidi na zinazoendelea kiuchumi zinatarajiwa kuanza majukumu mapya ya kudumu kuratibu uchumi wa dunia, taarifa ya Ikulu ya White House imeeleza.
Nchi hizo zinachukua jukumu hilo ambalo awali lilikuwa likishikiliwa na mataifa manane tajiri zaidi yaani G8.

Viongozi wa G20 wanafanya mkutano wa siku mbili huko Pittsburgh nchini Marekani.

Maafisa wa Jumuiya ya Ulaya wametangaza kuwa watabadilisha mfumo wa kuwateua viongozi wa Shirika la fedha duniani, IMF, ambapo nchi nyingine tajiri kama China zitashirikishwa.

China inashikilia asilimia tatu nukta saba ya kura katika IMF ikilinganishwa na Ufaransa ambayo huwa na asili mia nne nukta tisa, licha ya kwamba uchumi wa China umeimarika kwa asilimia 50 zaidi ya uchumi wa Ufaransa.

Mhariri wa BBC wa masuala ya biashara, Robert Peston, amesema nchi tajiri za kanda ya Amerika Kaskazini na Ulaya zimetambua kushirikisha maoni ya nchi nyingine kuhusu hali ya uchumi wa dunia, na hatua hii huenda ikazaa matunda kwenye mkutano wa leo.

Mabadiliko

Kwa sasa shirika la IMF linajumuisha nchi wanachama 186. Shirika hilo hutoa mikopo ya fedha kwa nchi zinazokumbwa na matatizo, mradi hizo zitafanyia mageuzi uchumi wao.

Awali IMF imekosolewa kwamba limekuwa kundi la mataifa tajiri ambayo hutoa sheria kwa nchi zinazojizatiti kuinua uchumi wao. hatua hii imepekea kushinikiza kuzipa nguvu nchi ambazo uchumi wao unakua kwa kasi.

Duru zaidi zinaarifu kuwa Marekani inanuia kupunguza wanachama wake katika bodi ya IMF kutoka 24 hadi 20, hatua ambayo huenda ikaisababishia Uingereza na Ufaransa kupoteza nyadhifa zao.

Wakati huo huo katika mji wa Pittsburgh, polisi walifyatua risasi za mipira kudhibiti maandamano. Mkutano wa G20 uliofanyika London mwezi Apirili vile vile ulikumbwa na vurugu za waandamanaji.

Vurugu zilianza pale waandamanaji walipojaribu kuelekea ukumbi wa mkutano huo bila kibali.

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na utekelezwaji wa maazimio katika kongamano hilo.

'' Bila kuweka juhudi zinazostahili, kuna tisho la kushuhudia ukuaji wa uchumi kwa kasi ndogo katika miaka ijayo'', alisema Bw Brown.

No comments:

Post a Comment