KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 27, 2009

Zimbabwe yakanusha Mugabe kuumwa


Maafisa nchini Zimbabwe wamekanusha taarifa kuwa rais Robert Mugabe ni mgonjwa, wakiziita taarifa hizo kuwa zenye nia ya uovu.

Gazeti la Times la Afrika Kusini limedai kuwa rais Mugabe alichukuliwa kwa siri na kupelekwa hospitali nchini Dubai kwa matibabu.

Lakini maafisa wa Zimbabwe wamesema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 85, amerudi nchini Zimbabwe baada kuwa likizo nchini Dubai, akiwa na afya njema.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anatarajiwa kuwasili nchini Zimbabwe siku ya Alhamis wiki hii kwa mazungumzo na rais Mugabe.

Msemaji wa Zuma amesema mkutano umepangwa kuendelea kama kawaida.

''Hatujapokea taarifa zozote rasmi kuhusu hali ya afya ya rais Mugabe, na kwa maana hiyo mipango yetu haijabadilika,'' amesema Vincent Magwenya.

UPUUZI MTUPU

Gazeti la Times liliripoti kuwa rais Mugabe amekuwa akifanyiwa matibabu maalum nchini Dubai.

Lakini maafisa wa Zimbabwe wamekanusha vikali madai hayo.

''Rais si mgonjwa, lakini alikuwa likizo,'' shirika la habari la Reuters lilimkariri afisa mmoja akisema.

''Amerudi nchini jana, na taarifa zote hizo ni upuuzi mtupu na mawazo dhaifu na ya uovu.''

Taarifa hizo zimekuja wakati rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akijiandaa kufanya ziara yake ya kwanza akiwa kama rais nchini Zimbabwe.

Zuma ni mwenyekiti wa sasa wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADEC), chombo kilichosaidia kufanikisha kuundwa kwa serikali ya ushirikiano ya Zimbabwe.

Chama cha Bwana Tsvangirai cha Movement for Democratic Change (MDC) kimekuwa kikitoa malalmiko mbambali kuhusu utekelezaji wa mgawanyo wa madaraka ikijumuisha uteuzi wa rais Mugabe kwa gavana wa benki kuu na mwanasheria mkuu.

Chama hicho kimesema uteuzi huo umekiuka moja ya kanuni zinazotakiwa katika serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

No comments:

Post a Comment