KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, August 18, 2009

Shambulio kuelekea uchaguzi Afghanistan


Mshambuliaji wa mabomu ya kujitoa mhanga amelipua bomu na kuua watu saba katika msafara wa vikosi vya kijeshi vya nchi za magharibi, katika mjii mkuu wa Afghanstan.
Tukio la bomu hilo ambalo ni la pili katika muda wa siku tatu limekuja katika kipindi ambacho ulinzi umeimarishwa katika mji mkuu Kabul kwa ajili ya uchaguzi hapo siku ya Alhamis.

Kikosi kinachoongozwa na NATO kimesema taarifa zinaashiria kuwa baadhi ya wanajeshi wake ni miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa, wakati Umoja wa Mataifa umesema wafanyakazi wake wawili wameuawa.

Saa chache mapema, roketi ilirushwa kuelekea katika makazi ya rais mjini Kabul, lakini hakuna aliyeripotiwa kujeruhiwa.

Mashariki mwa nchi, wanajeshi wawili wa Marekani walikufa katika shambulio la bomu la barabarani, jeshi la Marekani limesema.

Na hapo siku ya Jumanne kusini mwa Afghanstan, katika jimbo la Uruzgan, wanajeshi wawili wa Afghanstan walikufa wakati mshambuliaji wa bomu la kujitoa mhanga mwenda kwa miguu alipojilipua katika kizuizi cha ukaguzi.

Rais Hamid Karzai anatarajiwa kuchaguliwa tena kama rais hapo siku ya Alhamis, ingawaje wawakilishi wanasema anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Abdullah Abdullah. Wagombea kadhaa pia wanashiriki katika kinyang'anyiro hicho.

Hugh Sykes wa BBC mjini Kabul anasema matukio ya ulipuaji mabomu yanaelekea huenda yakawaogopesha watu kujitokeza kupiga kura.

Walioshuhudia wanasema shambulio hilo la Kabul lilitokea katika barabara yenye shughuli nyingi ya Jalalabad na kushambulia vikosi vya kijeshi vya kigeni karibu na soko lililojaa watu wengi, ambapo watoto waliikuwa ni miongoni mwa watu hamsini waliojeruhiwa.

Taliban wamedai kuhusika katika shambulio hilo.

Mwandishi mmoja aliyekuwako katika eneo la tukio aliwaona askari wa Uingereza waliokuwa wakifanya doria katika eneo hilo, wakikusanya kile kinachoonekana kuwa ni sehemu za miili ya binadamu kutoka katika paa la nyumba ya mtu mmoja muafghanistan.

''Niliona watu waliojeruhiwa na waliokufa wametapakaa kila mahali,'' muuza duka mmoja aitwaye Sawad ameliambia shirika la habari la Reuters.

Mlipuko huo ulisababisha moshi mzito angani, lakini haukuathiri sana mitaa yenye shughuli nyingi ya Kabul, anasema mwandishi wetu.

''Lilikuwa ni shambulio la kijitoa mhanga... Likilenga vikosi vya kijeshi vya kigeni,'' Mkuu wa police wa Kabul, Sayed Abdul Ghafar Sayedzada, aliliambia shirika la habari la AP.

Wafanyakazi wawili wa Umoja wa Mataifa wanaaminika kuuawa katika shambulio hilo.

''Nimestushwa na ninasikitika sana kutambua kuwa wawili kati ya wafanyakazi wangu ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio la kujitoa mhanga la leo,'' mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Kai Eide alisema katika taarifa.

Vurugu hizi za karibuni zinakuja wakati uchunguzi wa BBC umeonyesha kuna ushahidi wa ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi na ufisadi kuelekea siku ya uchaguzi wa rais.

Maelfu ya vitambuliho vya kupigia kura vimekuwa vikiuzwa na maelfu ya dola yamekuwa yakitolewa kama rushwa kununua kura.

Tume huru ya uchaguzi ya Afghanstan ambayo imekuwa ikisimamia mchakato wa uchaguzi imeshutumiwa kwa kushindwa kuzuia vitendo vitakavyoathiri uchaguzi.

Uchaguzi wa siku ya Alhamis utakuwa ni wa pili kumchagua rais tangu uvamizi ulioongozwa na Marekani mwaka 2001 ulioupindua utawala wa Taliban.

No comments:

Post a Comment