KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, August 21, 2009

Bingwa wa dunia wa mita 800 adhalilishwa


Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 Caster Semenya amedhalilishwa baada ya kutakiwa kufanyiwa uchunguzi juu ya jinsia yake, amesema mkuu wa idara ya michezo ya Afrika Kusini.
Leonard Chuene amesema bingwa huyo amechukuliwa kama vile ''mkoma''.

Mapema chama tawala nchini Afrika Kusini kiliwaasa wananchi kumuunga mkono na kumshangilia ''msichana wetu shujaa''.

Familia yake pia imesisitiza kuwa Caster Semenya ni mwanamke.
''Natambua kuwa ni mwanamke - nimemlea mwenyewe ,'' nyanya ya msichana huyo wa miaka 18 amesema.

Mama yake mzazi Dorcus Semenya ameliambia gazeti la Star kuwa, mashaka yaliyozuliwa juu ya jinsia ya mtoto wake yanatokana na ''wivu''.

''Iwapo utakwenda kijijini kwangu na kuuliza yeyote kati ya majirani zangu, watakueleza kuwa Mokgadi (caster Semenya) ni msichana,'' amesema.

''Wanajua kwasababu walinisaidia katika kumlea. Watu wanaweza kusema lolote wanalotaka lakini ukweli utabakia, kwamba mtoto wangu ni msichana. Sijali mambo kama hayo.''

Bwana Chuene, mkuu wa Idara ya Michezo Afrika Kusini amesema ataendelea kumtetea Semenya.

''Nitaendelea kufanya lolote lile, hata kama nitaondolewa Berlin, Ujerumani, lakini sitakubali kumwacha yule msichana adhalilishwe katika mtindo ambao amedhalilishwa, kwasababu hajafanya kosa lolote la jinai, '' amesema.

''Kosa lake lilikuwa ni kuwa amezaliwa jinsi alivyozaliwa.''

Katika taarifa ya chama tawala cha African National Congress (ANC) imeshutumu udadisi juu Semenya, aliyeshinda tuzo ya dhahabu katika mashindano dunia mjini Berlin hapo siku ya Jumatano, akiwaacha wapinzani wake wakichechemea.

''Maneno kama hayo yanaweza kuwawakilisha wanawake kama ni dhaifu,'' ANC imesema.

''Caster si mwanamichezo pekee wa kike mwenye umbo la kiume, na Shirikisho la Kimataifa la Wanamichezo lingetakiwa kulielewa hilo vyema zaidi,'' taarifa hiyo inasema.

Katika mahojiano na gazeti la Times la Afrika Kusini, nyanya wa bingwa huyo Maphuthi Sekgala mwenye umri wa miaka 80, amesema Semenya alikuwa akitaniwa alipokuwa mdogo kuwa ana muonekano wa kivulana.

Na pia alikuwa ni msichana pekee katika timu ya mpira wa miguu katika kijiji cha Fairlie, kilichopo katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini.

''Iwapo utani huo ulikuwa ukimuumiza moyo, aliweka maumivu hayo moyoni na hakuonyesha hisia zake,'' amesema.

No comments:

Post a Comment