KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 17, 2009

Chiluba aachiwa huru na mahakama


Mahakama nchini Zambia imetoa hukumu ya kutokuwa na hatia dhidi ya mashitaka ya ufisadi kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Fredrerick Chiluba, baada ya kesi iliyochukua kipindi kirefu.
Bwana Chiluba alishtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha dola 500,000 alipokuwa rais wa Zambia katika kipindi cha mwaka 1991 hadi 2001, lakini jaji ameamua kuwa hakuna ushahidi wa kuweza kuthibitisha fedha hizo katika fedha za serikali.

Mahakama ya Lusaka ilitoa uamuzi wake baada ya kusikiliza kesi hiyo katika kipindi cha miaka sita, kilichoambatana na hali mbaya ya kiafya ya Bwana chiluba mwenye umri wa miaka 63.

Kinga ya kisheria ya kutoshitakiwa kwa Bwana Chiluba iliondolewa mwaka 2003 na rais aliyechukua madaraka baada ya Bwana Chiluba, Levy Mwanawasa aliyefariki mwaka jana.

Bwana Chiluba amesema kesi hiyo ni uhasama wa kisiasa dhidi yake ulioendeshwa na Uingereza, iliyowahi kuitawala Zambia.

Katika kesi tofauti miaka miwili iliyopita, Mahakama Kuu nchini Uingereza ilimpata Bwana Chiluba kuwa na hatia ya wizi wa mamilioni ya dola za kimarekani, fedha za serikali ya Zambia kwa kutumia akaunti za bank nchini Uingereza zilizofunguliwa jijini London.

Bwana Chiluba amekataa kupokea nakala ya hukumu, akiita ni ''ubaguzi wa rangi''.

Mke wa Chiluba alihukumiwa kifungo gerezani mwezi Machi mwaka huu kwa kupokea fedha zilizoibwa wakati mumewe akiwa rais. Hata hivyo anakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

No comments:

Post a Comment