KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 15, 2012

Tetemeko lawafuata mabosi serikalini

Baada ya mawaziri wanane kutemwa ikiwa ni hatua ya kuwajibishwa, mabosi na watumishi wa umma wasio waadilifu na wasiowajibika katika majukumu yao sasa wametangaziwa tsunami. Tsunami hiyo ya kuwawawajibisha imetangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi ya Umma, Celina Kombani. Waziri Kombani ambaye ameteuliwa hivi karibu kuongoza wizara hiyo kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, alisema hayo wakati akizungumza na watumishi wa idara mbalimbali za serikali katika ziara yake ya siku tatu wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro. Kombani alisema kuwa, kwa kuanzia tsunami hiyo itapita kwa watumishi wazembe na wasio waadilifu katika mashirika na halmashauri ambazo zimepata hati chafu. “Hilo ni agizo la Rais, watumishi wote wazembe wajue kuna tsunami inakuja wakati wowote kuanzia sasa, wao ndio wamesababisha mawaziri wawajibike kisiasa wakati hawajafanya makosa,” alisema Kombani. Alisema kuwa watumishi hao wamekuwa wakishindwa kuwajibika na kusababisha mawaziri ambao hawajafanya makosa wawajibike kisiasa na kwamba kitu kama hicho hakitakuwepo tena kwani atakayezembea kwa nafasi yake ndiye atawajibishwa. Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Mashariki, Mkoani Morogoro, alisema kuwa kamwe serikali haitavumilia uzembe unaofanywa na watumishi na kwamba kuanzia sasa itamwajibisha mara moja yeyote atakayehusika na uzembe pamoja na kuisababishia serikali hasara. Alisema kuwa kwa kuanzia, tsunami hilo litapita kwa halmashauri zote ambazo zimeonekana kupata hati chafu katika ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuwachukulia hatua watumishi waliosababisha hali hiyo. Kombani alisema kuwa, wizara yake kuanzia sasa itakuwa ikipitia miradi ambayo serikali inaitolea fedha kuangalia kama inaendana na fedha zilizotolewa na ikibainika ni tofauti, mtumishi atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua kali ikiwemo ya kufikishwa katika vyombo vya sheria. Akizungumzia mikakati mingine aliyopanga kuifanya katika wizara hiyo, alisema ni kuhakikisha analimaliza tatizo la wafanyakazi hewa ambalo limeisababishia serikali hasara. “Hili la watumishi hewa ndio nitakufa nalo, wanaofanya hivyo wajue wamekalia kuti kavu na muda wowote watang’oka kwa hilo,” alisema Waziri Kombani. Aidha, Waziri Kombani, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa kupata hati safi kwa miaka mitano, huku akiwasisitizia watumishi wake kuongeza uadilifu na uaminifu katika utendaji wa kazi. Awali, wazee na viongozi mbalimbali wa dini wakizungumza katika mkuatano wa kumpongeza Waziri Kombani, walimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumteua tena katika nafasi ya uwaziri. Mei 4, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete, alilifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri na kuwatema mawaziri sita na manaibu mawaziri wawili. Waliotemwa ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk. Hadji Mponda. Manaibu mawaziri walioachwa ni Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athuman Mfutakamba (Uchukuzi). Mawaziri hao waligushwa na tipoti ya CAG na ripoti za wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC). Baadhi yao walituhumiwa kuhusika moja kwa moja katika matumizi mabaya ya fedha za umma na wengine walishindwa kusimamia wizara zao na kuisababishia serikali hasara. Aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, pia waliguswa na ripoti ya CAG na kamati za Bunge. Hata hivyo, Mkuchuika alihamishiwa Ofisi ya Rais (Utawala Bora) wakati Profesa Maghembe amehamishiwa Wizara ya Maji. Mkulo, ambaye anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), aitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma. Dk. Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi. Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo. Dk. Mponda, naye anadaiwa kushirishindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha. Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, George Mkuchika, ambaye anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika. Ngeleja, anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme, kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei. Maige, ambaye atauhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi. Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam; Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za mdororo wa uchumi.

No comments:

Post a Comment